Wanafunzi wa kidato cha sita |
Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), limeagiza kusitishwa kwa ugawaji wa vyeti
vya kidato cha sita kwa wanafunzi waliohitimu mwaka 2015, huku vile
vilivyokwisha kugawa kwa watahiniwa hao vikitakiwa kurejeshwa kwenye chombo
hicho.
Hali hiyo imeibua utata
mkubwa, huku baadhi ya wadau wakiwamo maofisa elimu, wakihisi hatua hiyo ya
Necta huenda inalenga kuvibadili vyeti hivyo kutoka kwenye mfumo wa wastani wa
alama (GPA), kwenda kwenye ule wa jumla (division).
Ofisa Elimu Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda, alipoulizwa kama
amepokea agizo hilo, alithibitisha kuwa shule zote za mkoa huo zenye kidato cha
tano na sita zimepewa taarifa ya kutakiwa kurudisha vyeti hivyo Necta.
Alisema sababu ya kuvirudisha vyeti hivyo anadhani ni kufanya
mabadiliko kutoka GPA na kurudi kwenye divisheni.
Ofisa Elimu Mkoa wa Arusha, Nestory Mloka, alisema amepata barua
ya maelekezo hayo kutoka Necta ikimuelekeza kuwataka maofisa elimu wilaya
wawasiliane na wakuu wa shule za kidato cha tano na sita wasigawe vyeti vya
wanafunzi waliohitimu mwaka 2015.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Matthew iliyoko Kongowe,
Mkuranga mkoani Pwani, Abraham Shafuri, naye alikiri kuwapo kwa agizo la Necta
la kusimamisha utoaji wa vyeti hivyo kwa wahusika.
Alisema aliambiwa na maofisa wa Necta kuwa vyeti hivyo
vinatakiwa kurejeshwa kwenye baraza hilo na kwamba sababu zilizotolewa ni kuwa
kuna marekebisho kidogo yanapaswa kufanyika.
“Nilichoambiwa ni
kwamba shule karibu zote za Dar es Salaam zimesharejesha vyeti hivyo na kwamba
kwa sisi wa mkoa wa Pwani, maofisa hao watapita kuvichukua lakini hatujui ni
lini watakuja,” alisema Shafuri.
Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk, Charles Msonde,
alipoulizwa alikanusha vikali madai hayo, akisema vyeti hivyo
havitabadilishwa kutoka kwenye mfumo wake bali vimesitishwa kugawanywa ili
baraza lijiridhishe na baadhi ya vitu.
“Vyeti hivi baraza
limevigawa hivi karibuni na lilichofanya sasa limezuia kwanza shule zisigawe
mpaka litakapotoa maelekezo mengine, msingi huo wa kuzuia uko kwenye hoja ya
kuhakikisha tu kwamba linajiridhisha kwenye takwimu zake kama zimekaa sawasawa
katika vyeti vilivyokwenda kila shule.
“Baadhi ya vyeti
kwenye mkoa wa Dar es Salaam vipo Necta, lakini kwenye mikoa mingine yote viko
shuleni,” alisema Dk Msonde na kuongeza;
“Kama mkuu wa shule
alikuwa amegawa vyeti viwili, vitatu kabla havijarejeshwa baraza ni suala
jingine, lakini kiujumla kinachofanywa na baraza hapa ni kuhakiki cheti hiki,
kama vimekaa kama utaratibu wetu ulivyo.”
Alisema suala la kubadilisha kutoka kwenye GPA kwenda kwenye
divisheni halipo na kwamba matokeo yaliyotangazwa kwa utaratibu wa GPA vyeti
vyake vitaendelea kuwa katika mfumo wa GPA na matokeo yaliyotangazwa kwenye
utaratibu wa divisheni vyeti vyake vitabaki kuwa kwenye divisheni.
Alisema kwa wale ambao
tayari wako nje ya nchi, hakuna atakayeathirika na kama baraza likihitaji cheti
chake litafanya utaratibu wa kukipata.
No comments:
Post a Comment