Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto
Dkt. Faustine Ndugulile amethibitisha kuwa hakuna mtu aliyethibitika kuwa na
ugonjwa wa EBOLA hapa nchini wala hakuna ugonjwa huo hapa Tanzania.
“Napenda kuwatoa hofu watanzania kwamba hakuna ugonjwa wa EBOLA
na wala hakuna mtu aliyethibitika kuwa na ugonjwa huo, hivyo tuendelee na
shughuli za kujenga Taifa ila tunatakiwa tuchukue tahadhari za kujikinga juu ya
ugonjwa huu” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha, Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika kuchukua tahadhari juu
ya ugonjwa wa EBOLA usiingie nchini Serikali imeweka vifaa vya kupima joto la
mwili (themo scaner) pia wapo wataalamu wa Afya ambao wanauliza hali ya
wageni wanaoingia katika mipaka yote inayoizunguka nchi yetu ili kuzuia ugonjwa
huo kuingia.
Dkt. Ndugulile amesisitiza kuwa, Serikali haijafunga mipaka ya
nchi kwa sababu ya kujikinga na EBOLA.
“Tanzania hatujafunga mipaka na hatuwezi kufunga biashara za mipakani
ila tumeimarisha ufuatiliaji wa watu wanaoingia nchini hususani maeneo ya
viwanja vya ndege na mipaka mingine yote.”
Mbali na hayo Dkt. Ndugulile ameitaka mikoa yote iliyo mipakani
kudhibiti watu wote wanaoingia nchini kwa njia za panya ili kuepusha uingizaji
wa ugonjwa huo kwa wananchi huku akiwataka wafanyabiashara wa mipakani
kutoa ushirikiano ili kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani ambaye pia
ni Afisa wa kushughulikia magonjwa ya kuambukiza Dkt. Grace Saguti amesema kuwa
Wananchi wanatakiwa kupata elimu juu ya kujikinga na ugonjwa huo.
“Elimu inahitajika ya kutosha kwa wananchi wote hasa katika
kufichua wagonjwa wa Ebola kama watagundulika hasa wanaotoka nje ya nchi ili
kupata msaada kutoka kwa watoa huduma za afya walio yao juu ya kujikinga na
ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment