Friday, 25 May 2018

CAF, UEFA WAKOSHWA NA MAANDALIZI YA TANZANIA



Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) wamesifu maandalizi ya Tanzania kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakayofanyika nchini mwakani.



Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano ya Kimataifa cha UEFA, Eva Pasquier alisema kwa siku nne walizofanya ukaguzi, kasi ya maandalizi inatia moyo.

"Kwa siku chache tulizokuwa hapa tumejifunza mengi na tumeona juhudi za Tanzania katika kuleta maendeleo ya soka la vijana na wanawake.

Tunashukuru kwa mapokezi mazuri tuliyopata na tunaamini huu ni mwanzo mzuri wa ushirikiano baina ya UEFA, CAF na Tanzania," alisema Pasquier.

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya CAF, Junior Binyam alisema mchakato wa ukaguzi umekuwa wa mafanikio.

"Tumefanya ukaguzi wa masuala mbalimbali ikiwemo viwanja vitakavyotumika kwa mechi na mazoezi, hoteli pamoja na miundombinu mingine kama ya usafirishaji.

Kiujumla mwelekeo ni mzuri na tutatoa mapendekezo ambayo tutaipa kamati ya maandalizi ya ndani ambayo itayafanyia kazi kabla ya ukaguzi mwingine kufanyika," alisema Binyam.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema shirikisho pamoja na kamati ya maandalizi wanajiandaa kufanyia kazi mapendekezo watakayopewa na timu hiyo ya ukaguzi kisha kuyafanyia kazi.

"Moja ya masharti ni kuyaandaa mashindano hayo katika miji miwili tofauti lakini tumejaribu kuwaelezea hali halisi kuwa miundombinu yetu hairuhusu hivyo wametuelewa na kilichobaki kwa sasa ni kusubiri nini watakachotuelekeza ili tukifanyie kazi," alisema Karia.

No comments:

Post a Comment