Tume ya kuhakiki mali
za Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyoundwa na Rais John Magufuli, imebaini madudu
ukiwamo utapeli na usimamizi mbaya wa mali hizo.
Akikabidhi ripoti hiyo
kwa Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Mwenyekiti wa Tume
hiyo, Dk. Bashiru Ally, amesema tume yake pia ilibaini usimamizi mbovu wa mali
za chama.
Akielezea namna tume
hiyo ilivyofanya kazi, Dk. Bashiru amesema pamoja na mambo mengine, tume
iliangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wa mali,
imekusanya ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya mikakati na ushauri wa
kusimamia mali za chama.
Katika ripoti hiyo,
Dk. Bashiru ameeleza tume imebaini uwepo wa upotevu mkubwa wa mali za chama
uliosababishwa na mikataba mibovu, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali,
utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama.
“Uhakiki huo
umefanyika kwa kutembelea maeneo yenye mali za chama, kuwahoji watu mbalimbali
wakiwamo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa, upitiaji wa
nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya
uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo,” amesema.
Kwa upande wake Rais
Magufuli ameipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya na amesema ripoti
hiyo itawasilishwa katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kwa
ajili ya kufanyiwa uamuzi.
“Nilipokuwa nateua
tume hii, nilikuwa najua ugumu wa kazi, nilikuwa najua kuwa mtapata shida
kwenda kuwahoji watu licha ya kwamba niliwapa uhuru wa kumhoji mtu yeyote na
mmefanya kazi nzuri sana, kilichobaki sasa ni kuifanyia kazi” amesema Rais
Magufuli.
No comments:
Post a Comment