Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya
Ndani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi waangalie umuhimu wa kutumia
mifumo ya ulinzi wa miji ya kieletroniki (City Surveillance System) ili
kupunguza uhalifu na kuongeza usalama wa wananchi na mali zao.
Ametoa agizo hilo jana (Alhamisi, Mei 24, 2018) wakati
akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na
viongozi wa Jeshi la Polisi kwenye viwanja vya Mbweni, wilayani
Kinondoni, mkoani Dar es Salaam baada ya kuzindua vituo vya polisi vya
kisasa vya Mburahati, Kiluvya - na
Mbweni.
“Katika suala zima la kuimarisha usalama, napenda niwape
changamoto Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi ili zitoe
kipaumbele kwenye matumizi ya City Surveilance System (CCTV). Usimikaji wa
mifumo hiyo utasaidia kupunguza uhalifu na kuongeza usalama wa wananchi na mali
zao,”
Amesema.
Waziri Mkuu amesema tayari Jiji kama Nairobi la nchini Kenya
linatumia mifumo ya aina hiyo na kwamba uwepo wa mifumo hiyo, na haoni ni kwa
nini Tanzania bado haijawa na mifumo kama hiyo.
Amesema uwepo wa mifumo hiyo, utasaidia si tu kutambua kwa
wepesi wahusika wa matukio ya uhalifu kama vile ukwapuaji, wizi wa magari na
uharibifu wa mali, bali pia utaongeza shughuli za kibiashara na utalii.
"Tanzania hatujaanza kutumia mifumo hii lakini ifike
mahali, tuanze kubadilika. Tafuteni wataalamu wenye ujuzi watufungie mifumo hii
ili iwe rahisi kufuatilia matukio mbalimbali. Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani fuatilia mifumo hii ili tuanze na majiji yetu na tuweze kufuatilia
matukio ya kihalifu barabarani na mitaani", Amesema Waziri Mkuu.
"Nitoe rai kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la
Polisi wachukue hatua za haraka kurahisisha upatikanaji wa matumizi ya mifumo
hiyo hususan katika majiji yetu kwa ajili ya kuimarisha usalama wa watu na mali
zao," Amesema.
Mapema, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Yusuf Masauni alimshukuru Rais Dkt, John Pombe Magufuli kwa kukubali kutoa
kiasi cha sh.bilioni 10 kwaajili ya ujenzi wa nyumba za polisi.
Alisema kutokana na fedha hizo, nyumba takriban 400 za askari
polisi, zinatarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa vituo hivyo vitatu, Inspekta
Jenerali wa Polisi, Simon Sirro alisema ujenzi wa kituo cha Mburahati
umegharimu sh. bilioni 1.2, Kiluvya (sh. milioni 227) na Mbweni (sh. milioni
667).
Alisema ujenzi wa vituo hivyo umeshirikisha wananchi wa maeneo
husika, Jeshi la Polisi na wadau werevu ambao ni walipakodi wazuri na wazalendo
zikiwemo taasisi na watu binafsi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment