Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt Faustine Ndugulile
Watoto wa kike nchini wameaswa kujitambua,
kujiamini na kujilinda dhidi ya vishawishi vinavyosababisha matukio maovu ya
Ukatili wa Kijinsia zikiwemo mimba na ndoa za utotoni na kusababisha kukatisha
ndoto zao za kupata haki ya kuendelezwa na elimu bora kwa manufaa yao, family
na Taifa.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe. Dkt Faustine Ndugulile Wilayani Kahama Mkoani
Shinyanga wakati wa uzinduzi wa klabu za wasichana katika shule ya Sekondari ya
Mwendakulima.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa vitendo vya
ukatili wa kijinsia vinazidi kushamiri katika jamii zetu hususan katika meneo
ambayo bado wanafuata mila na desturi ambazo zinamkandamiza mtoto wa kike na
mwanamke.
Ameongeza kuwa namna bora ya kupambana na
ukatili wa kijinsia ni kwa watoto wa kike kutonyamaza pale ambapo wanafanyiwa
vitendo vya ukatili hasa kuozeshwa na kushawishiwa kuingia kwenye mahusiano ya
kingono katika umri mdogo: mambo yanayosababisha mimba na ndoa za utotoni.
“Kila mtu aunge mkono juhudi zetu za pamoja za
kutokomeza mimba na ndoa za utotoni kwa kuacha usiri na kushirikiana kutoa
taarifa ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa mamlaka zilizopo“
alisiistiza Dkt. Ndugulile.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe.
Fadhili Nkulu amesema kuwa Wilaya yake inaendelea kushirikiana na jamii na
wadau wa maendeleo katika kuendeleza juhudi za Serikali za Kupambana na Vitendo
vya Ukatili wa Kijinsia zikiwemo mimba na ndoa za utotoni ili kuwapatia watoto
wa kike haki yao ya kuendelezwa na kuwaandaa kuwa nguvu kazi bora ya Taifa la
uchumi wa kati na wa viwanda.
Naye mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari
Mwendakulima Mwajuma Salum amesema klabu za wasichana zinawasaidia sana watoto
wa kike kujitambua kwa kupata elimu zinazowawezesha kupamabana na vitendo vya
ukatili wa kijinsia hasa mimba na ndoa za utotoni.
Aidha, ameeleza kuwa mbinu wanazopata
zinawasaidia kuishi na wanafunzi wenzao wa kiume kama kaka na dada wakiwa na
jukumu la kuwalinda na kuwapa kuwashauri kuzingatia wajibu wao katika masomo.
No comments:
Post a Comment