Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akiagana na wananchi wa Wilaya ya Maswa mara baada ya mkutano wa Hadhara uliofanyika Uwanja wa Nguzo Nane mjini Maswa.
|
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe.Samia Suluhu Hassan amewahimiza wananchi mkoani Simiyu kuchangia ujenzi wa
miundombinu ya elimu ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika maendeleo ya
Sekta ya Elimu.
Mhe.Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati
akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu kwenye Mkutano
wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Nguzo Nane wakati wa ziara yake mkoani humo.
Amesema Serikali imeamua kutoa elimu bila malipo na
kuwapunguzia wazazi mzigo wa kulipia gharama za karo na michango mbalimbali ya
uendeshaji wa shule lakini suala la kuchangia ujenzi wa miundombinu ya elimu
wananchi wanapaswa kuunga kuchangia ili kuunga mkono juhudi hizo.
“ Tunapeleka fedha katika shule zote za Msingi na
Sekondari ili wanafunzi waweze kusoma vizuri lakini kwenye suala la ujenzi wa
matundu ya vyoo, madarasa, maabara pamoja na kwamba Serikali ina wajibu wa
kufanya hayo na ninyi wananchi mnao wajibu wa kusaidia kufanya hayo” alisema
Mhe. Makamu wa Rais.
Wakati huo huo Mhe.Makamu wa Rais ameipongeza Wilaya
ya Maswa kwa kuongeza ufaulu kutoka asilimia 45 hadi asilimia 75 kwa mwaka 2017
na akakemea vikali tabia ya wanaume wanaoua ndoto za watoto wa kike kwa kuwapa
mimba , ambapo amesema jicho la Serikali liko kwa watoto wa kike na
itawachukulia hatua kali wote watakaobainika kufanya hivyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt.Seif
Shekalaghe amesema watoto wa kike 28 wameripotiwa kuwa na mimba katika kipindi
cha mwezi Desemba 2017 hadi sasa na Serikali ya Wilaya kupitia Operesheni
tokomeza Mimba imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 15 na kati ya hao wawili
wamehukumiwa miaka 30 jela kila mmoja.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi Mbunge wa Jimbo la
Maswa Mashariki ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini , Mhe.Stanslaus Nyogo
amewashukuru viongozi wa Wilaya kuleta mafanikio katika elimu ikiwa ni pamoja
na ongezeko la ufaulu.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan mara baada ya kufungua Jengo la
Upasuaji la Upasuaji Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo limepewa jina lake
“SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” amewataka Watumishi wa Afya kufanya
kazi kwa bidii.
Aidha, amesema Serikali itahakikisha inaboresha
huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya Afya katika kila kata na
kuboresha huduma za Afya ya Mama na Mtoto ili kupunguza Vifo vya mama na mtoto.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI,
Mhe.Josephat Kandege amesema Serikali imekusudia kujenga vituo vya Afya 286
kufikia mwisho mwa mwaka 2017/2018 lengo likiwa ni kuboresha utoaji
wa huduma za afya kwa kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika Hospitali za
Wilaya.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mhe.Mashimba
Ndaki amesema pamoja na kuendelea kuboresha sekta ya Afya kwa kujenga
miundombinu, ni vema Serikali ikaajiri watumishi wa Idara ya Afya kukabiliana
na upungufu uliopo.
Mhe.Makamu wa Rais amemaliza Ziara yake Wilayani
Maswa ambapo amefungua Jengo la Upasuaji la Upasuaji Hospitali ya Wilaya ya
Maswa ambalo limepewa jina lake “SAMIA SULUHU HASSAN OPERATING THEATER” na
kuzungumza na wananchi katika Uwanja wa Nguzo Nane.
No comments:
Post a Comment