Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile
Na Beatrice Lyimo - MAELEZO, DODOMA
Serikali imewataka wananchi kutoa taarifa
kuhusu hospitali zinazotoza fedha kwa ajili ya matibabu kwa akina mama wajawazito
ili kuweza kuchukua hatua muhimu kukomesha hali hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni Mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto
Dkt. Faustine Ndugulile wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu
Hawa Chakoma lililohusu matibabu bure kwa mama wajawazito.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa mama wajawazito
ni moja ya makundi maalumu wanaostahili kupata huduma za matibabu bure kama
ilivyooneshwa katika mwongozo na uchangiaji wa huduma za afya wa mwaka 1997.
"Mwongozo umeweka bayana kuwa kina mama
wajawazito ni haki yao kupewa huduma zote bila malipo na sio zile tuu
zinazohusu huduma za ujauzito katika mwongozo uliopitiwa mwaka 2009/2010
imetamkwa bayana kuwa huduma za afya kwa mama wajawazito ni bure, ikiwa na
maana kwamba mara tu mwanamke anapokuwa na ujauzito huduma zote kuanzia
kliniki ya wajawazito, pale anapogundulika maradhi yoyote, pamoja na huduma
ya kujifungua sanjali na kumuona daktari, kupatiwa vipimo, kupewa dawa na
kufanyiwa upasuaji pale inapohitajika kufanya hivyo" amefafanua Dkt.
Ndugulile.
Aidha, Dkt. Ndugulile amesema kuwa Wizara
imeanzisha utaratibu wa kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa
vinavyohitajika wakati wa kujifungua ambapo watapewa akina mama wajawazito
wanapokaribia kujifungua.
Hata hivyo, Dkt Ndugulile amesema kuwa kwa
sasa kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa akina mama kujifungua katika vituo vya
afya ambapo zaidi ya asilimia 60 ya akinamama wanajifungulia kwenye vituo vya
afya.
Mbali na hayo, Serikali imezitaka
Halmashauri zote nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera hiyo ili
akina mama wajawazito wapate huduma za matibabu bure kama Mwongozo wa
Uchangiaji wa mwaka 1997 na Sera ya Afya ya mwaka 2007 inavyoelekeza.
|
No comments:
Post a Comment