Waziri mkuu Kassim
Majaliwa amemsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Misungwi
Bw. Alphonce Sebukoto na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.
Amechukua hatua hiyo
baada Mwanasheria huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni
pamoja na kushindwa kuishauri vema halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya
sh. milioni 279.
Waziri Mkuu
amemsimamisha kazi Bw. Sebukoto leo (Jumatatu, Februari 19, 2018) wakati
akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika siku ya
tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
“Mwanasheria utasimama
kazi kuanzia leo na tuhuma zako zitachunguzwa kikamilifu na vyombo husika na
uchunguzi ukibaini kama huna kosa utarudi kazini. Hatuta kuonea lakini hatuwezi
kukuvumilia kwa utaratibu huo ulioufanya.”
Amesema mwanasheria
huyo Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya ukurugenzi aliidhinisha
malipo ya sh.milioni 279 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa
Halmashauri hiyo Bw. Anthony Bahebe.
Waziri Mkuu amesema
Bw. Bahebe aliishtaki halmashauri hiyo akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi
ya ukandarasi wa mradi wa maji Igenge uliojengwa na kampuni ya ukandarasi ya
Seekevim.
Amesema mradi huo
ulianza 2014 na ulitakiwa ukamilike 2015. Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo
hayo wakati ambao tayari hati maalumu ya uwakilishi ilikuwa imekwisha tangu
Desemba 2015.
“Mwanasheria amemlipa
Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri baada ya kuifikisha
Halmashauri yake Mahakamani. Amemlipa fedha wakati kazi yenyewe ilikuwa
haijaisha na aliharakisha malipo hayo kipindi ambacho Mkurugenzi hayupo.”
Waziri Mkuu amewakumbusha
watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika
utekelezaji wa majukumu yao. Amesema fedha alizolipwa Bw. Bahebe zingeweza
kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri
hiyo.
Awali, Waziri Mkuu
alifungua mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi
Mitindo iliyoko wilayani Misungwi na kisha alikagua ujenzi wa vyumba vya
madarasa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 19, 2018.
No comments:
Post a Comment