Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Elias John Kwandikwa
(kushoto) akisisitiza jambo kwa watendaji
wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Tanga mara baada ya
kukagua barabara ya Turiani- Mziha- Handeni yenye urefu wa kilomita 108
jumatatu Februari 12, 2018. Kulia ni Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga,
Mhandisi Alfred Ndumbaro
Naibu Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Elias John Kwandikwa (kushoto)
akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Wilaya ya Handeni wakiongozwa na Mkuu wa
Wilaya hiyo, Godwin Gondwe (wa pili kushoto) mara baada ya kukagua
barabara ya Handeni- Manyara yenye urefu wa kilomita 88 jumatatu Februari
12, 2018.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Elias John Kwandikwa
(kushoto) akijadiliana jambo na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe
(katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Korogwe, William Makufye wakati wa
ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara Wilayani humo jumatatu
Februari 12, 2018.
Serikali imesema ipo mbioni kuanzisha mfumo wa utambuzi na usajili wa barabara zote nchini, hatua inayolenga kuziwezesha barabara zote kujengwa katika viwango vinavyofafana na ubora wa huduma ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi hususani wa maeneo ya vijijini.
Hayo yamesemwa leo Wilayani Handeni Mkoani Tanga na
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa wakati wa
ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara katika Wilaya za Handeni,
Kilindi na Korogwe.
Kwandikwa alisema ili kutekeleza adhma hiyo,
Serikali imekusudia kuiwezesha Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini
(TARURA) kwa kuiongezea uwezo wa vitendea kazi na waatalamu wa kutosha ili
kuhakikisha kuwa miradi ya barabara iliyopo katika Halmashauri zote nchini
inakuwa na chombo maalum cha usimamizi.
“Ni wajibu wa Watendaji wote kushirikiana katika
kusimamia miradi ya barabara, kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa TARURA
ikiwemo kuipata fedha pale inapokwama katika kutekeleza wajibu wake hususani
katika maeneo korofi yanayohitaji fedha maalum” alisema Kwandikwa.
Alisema kukamilika kwa miradi ya barabara katika
maeneo mengi ya vijijini kutawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika
shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uzalishaji na usafirishaji wa mazao na
pembejeo na hivyo kuvutia uwekezaji katika miradi mikubwa ya maendeleo.
Aidha Kwandikwa alisema ili kutekeleza vyema
majukumu yake, ni wajibu pia wa TARURA kujisogeza karibu zaidi kwa jamii
ikiwemo kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi na Viongozi mbalimbali katika
Mamlaka ya Serikali za mitaa, hatua inayolenga kujenga uelewa wa mamlaka,
wajibu na majukumu ya taasisi hiyo.
Aliongeza kuwa asilimia 80 ya uwezeshaji wa uchumi
katika maeneo ya vijijini unategemea upatikanaji wa miundombinu ya barabara za
uhakika, hivyo ni wajibu wa TARURA kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki
kikamilifu katika shughuli za kuinua uchumi pasipo kukabiliwa na changamoto
zisizo na ulazima.
Akifafanua zaidi Kwandikwa alisema Serikali ipo
tayari wakati wowote kutoa ushirikiano unaohitajika ikiwemo kupokea ushauri,
mapendekezo na maoni kuhusu hatua mbalimbali zinazopaswa katika kuboresha na
kusimamia miundombinu ya barabara inayosimamiwa na taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin
Gondwe alisema Wilaya yake imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha kuwa
sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinafuatwa katika usimamizi wa
miundombinu ya barabara kwa kuwa hatua itasaidia kuleta maendeleo ya haraka kwa
wananchi.
“Wilaya imejipanga kikamilifu katika kusimamia
sheria ikiwemo kudhibiti mifugo inayovuka kutoka upande mmoja wa barabara
kwenda mwingine, kwa kuwa mara nyingi imekuwa ikichangia uharibifu wa miundombinu
ya barabara zetu” alisema Gondwe.
No comments:
Post a Comment