Mgodi wa dhahabu wa Acacia Bulyanhulu umezindua na kukabidhi
maktaba iliyogharimu shilingi milioni 22.6 kwenye shule ya sekondari
Bulyanhulu iliyopo katika halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani
wa Shinyanga kwa lengo la kusaidia wanafunzi na walimu katika
kuboresha ubora wa elimu inayotolewa.
Maktaba hiyo imezinduliwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
Msalala Bw , Simon Berege na kuhudhuriwa na kaimu
Meneja mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu,Elias Kasitila.
Akizungumza wakati uzinduzi huo, Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi
Bulyanhulu,Elias Kasitila alisema wakati wakitafakari namna ya kuinua
taaluma ya wanafunzi waliona ni vyema wakaimarisha usomaji wa wanafunzi kwa
kuwekeza kwenye maktaba ambayo itasaidia kuboresha upatikanaji wa
elimu kwa wanafunzi kutoka kwa jamii inayouzunguka mgodi huo.
Alisema kupitia mpango wa Acacia wa maendeleo ya jamii wameamua
kushirikiana na shirika la kimataifa la Read International kuboresha jengo moja
la shule hiyo na kuliwekea samani kwa ajili ya matumizi ya maktaba ambayo
itawasaidia wanafunzi na walimu kwa kiasi kikubwa.
“Misaada inayotolewa na Acacia katika sekta ya elimu ni sehemu ya sera ya
wajibikaji kwa jamii ya kampuni inayojikita katika kuhakikisha jamii inakuwa
endelevu kupitia sekta ya elimu na sera hiyo inachangia moja kwa moja maono ya
taifa hadi kufikia mwaka 2025 na malengo ya nchi ya kuleta maendeleo endelevu
kwa kuhakikisha jamii inapata elimu iliyo bora”,alisema Kasitila.
Mwakilishi wa shirika la Read International linalojihusisha na masuala ya
elimu,Esther Kalwinzi alisema pesa ambazo zimetolewa na mgodi huo ni shilingi
milioni 22.6 kwa ajili kukarabati darasa kuwa maktaba.
Kwa upande wake,mgeni rasmi katika hafla hiyo,Mkurugenzi wa Halmashauri ya
msalala , Simon Berege umeushukuru mgodi huo pamoja na
shirika la Read International kwa kufadhili maktaba hiyo ya kisasa kwenye shule
hiyo na kwamba itasaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kujisomea na kujenga uwezo
mkubwa kwenye masomo yao.
Kikubwa zaidi ninacho wasisitiza wanafunzi kuzingatia masomo na pia
wazazi tambueni elimu ndiyo urithi pekee wa kudumu na wenye kubadilisha maisha
ya mtoto kutoka hali ya chini ya umasikini kuja juu zaidi
kimaisha”Alisisitiza Berege.
Hata hivyo mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo Mussa Rajabu alisema
kuzinduliwa kwa maktaba hiyo kutaleta chachu ya kupenda kujisomea
zaidi na kwamba itawasaidia kufanya vizuri kwenye masomo yao.
No comments:
Post a Comment