Hospitali ya rufaa Mkoani Geita inayojengwa Mtaa wa Magogo kata ya
Bombambili mjini Geita inatarajiwa kuhudumia wagonjwa zaidi ya elfu moja wa nje
na zaidi ya 480 watakaokuwa wakilazwa.
Akizungumza na waandishi wa habari walioambatana na Mwenyekiti wa bodi
teule ya hospitali hiyo, Kaimu Meneja wa Wakala wa majengo mkoani Geita
Mhandisi Glads Jefta alisema katika hatua ya kwanza ya ujenzi wanaendelea na
ujenzi wa majengo manne na wanatarajia kukamilisha baada ya miezi 9 ambapo
umefikia asilimia 35.
“Tunatarajia hospitali hii
itakapokamilika itahudumia idadi ya wagonjwa wa nje zaidia ya elfu moja na wa
kulazwa mia nne na themanini na tunaamini ndani ya muda wa miezi
mitatu ambayo tumeomba kuongezewa tutakuwa tumekamilisha ujenzI” Alisema
Mhandisi Glads.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali Teule ya mkoa wa Geita Bw ,Simon
Rweyemamu alisema matarajio walitarajia Hospitali hiyo ingekamilika ndani ya
miezi 9 lakini kukosekana kwa umeme na maji ndio sababu zilizokwamisha mradi
huo kwa kuwa Mkandarasi amekuwa akinunua maji kutoka nje na wakati mwingine
kutumia mafuta kwa ajili ya jenereta.
Kaimu mganga mkuu wa Mkoa wa Geita Dr Joseph Odero alisema hospitali ya
rufaa ya sasa ambayo ilikuwa ya wilaya ni ndogo kwa kuwa ina uwezo wa kuhudumia
wagonjwa 150 hadi 200 na wale wa kulazwa 200 hadi 250 na kwamba
hali ya wagonjwa kwa sasa ni kuanzia 300 hadi 350 hivyo kukamilika kwa
hospitali hiyo ya rufaa kutasaidia kukabiliana na changamoto ya wingi wa
wagonjwa
Mradi wa ujenzi wa hospitali ya rufaa kwa sasa umefikia asilimia 35
kwa hatua ya kwanza ambayo inatarajia kugharimu kiasi cha Sh Bilioni 5.9
|
No comments:
Post a Comment