Waziri mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza kamanda wa TAKUKURU mkoa
wa Mtwara Bw. Stephen Mafipa kumtafuta popote alipo na kumkamata
aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi Bw. Fortunatus
Kagoro kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.
Mbali na Bw. Kagoro pia Kaimu Mweka Hazina Bw. Heri Hamad Afisa
Mipango Bi Teresia Nsumba nao ameagiza wakamatwe na baada ya uchunguzi
watakaobainika kwamba hawajahusika na ubadhilifu huo watarudishwa kazini.
"Lazima fedha za Serikali zitumike kama ilivyokusudiwa."
Watendaji hao wanadaiwa kutumia sh. bilioni 1.8 zilizotolewa na
Serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Mji wa Masasi kwa
kuchora mchoro na kujenga msingi katika maeneo mawili tofauti.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Februari 26, 2018)
wakati akizungumza na watumishi na Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Masasi na
Halmashauri ya wilaya ya Masasi akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani
Mtwara.
Amesema mwaka 2014 Serikali ilipeleka sh milioni 575
wilaya Masasi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri hiyo na fedha hizo
ziliishia kutumika katika hatua za maandalizi ya awali ikiwa ni pamoja na
kutengeneza michoro ya jengo.
Waziri Mkuu amesema 2016/2017 Serikali ilipeleka tena sh.
bilioni 1.25 kwa ajili ya ujenzi huo, ambapo Halmashauri hiyo ilienda kutafuta
eneo lingine na kufanya tena shughuli zilizokuwa zimefanyika na kuanza ujenzi
ambao umeishia katika msingi na fedha zimeisha.
Pia amewataka watendaji hao kutotumia fedha za makusanyo ya
ndani kwa ajili ya kuziba pengo la fedha za mradi huo ambazo baadhi yake
hazijulikani zilipo na amewaagiza Madiwani kutoruhusu jambo hilo.
"Madiwani msikubali kutumia fedha za makusanyo ya ndani
kupeleka kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo ambayo tayari Serikali ilishatoa
fedha ya ujenzi wake.
Amesema Serikali inahitaji kuona fedha za maendeleo
zinazopelekwa katika Halmashauri mbalimbali nchini zinatumika kama
ilivyoelekeza na si vinginevyo na Serikai haitakuwa na mzaha kwa mtumishi
atakayezitumia vibaya.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 26, 2018.
No comments:
Post a Comment