Serikali imesema
mwalimu wa sekondari kufundisha shule ya msingi si kushushwa cheo na wala si jambo
la ajabu.
Taarifa ya mkuu wa
kitengo cha mawasiliano Ofisi ya Rais (Utumishi), Florence Lawrence imesema
Serikali kuwapangia baadhi ya walimu wa sekondari kufundisha shule za msingi ni
moja ya hatua za kuongeza ufanisi na kuleta mgawanyo sawa wa walimu katika
shule hizo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk Laurean Ndumbaro amekaririwa katika
taarifa hiyo iliyotolewa leo Februari 20,2018 akisema hatua hiyo haimaanishi
kuwa walimu wanaotoka katika shule ya sekondari kwenda kufundisha msingi
wameshushwa cheo.
Dk Ndumbaro ametoa
ufafanuzi huo katika kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa
Makambako.
Amesema lengo la
Serikali ni kuondoa upungufu wa walimu katika shule za msingi na kuimarisha
utoaji wa elimu.
Katibu mkuu ameainisha
kuwa sifa za kufundisha na kiwango cha elimu zinaendana na mabadiliko
yanayotokea duniani, hivyo mwalimu mwenye elimu ya kiwango cha Shahada ya
kwanza kufundisha shule ya msingi isionekane ni jambo la ajabu.
Dk Ndumbaro amewaambia
watumishi wa umma kuwa, maendeleo katika sekta yoyote, ikiwamo ya elimu
yanakuja na mabadiliko hivyo wayapokee na kufanya kazi ili kufikia lengo.
No comments:
Post a Comment