Tuesday, 21 March 2017

SERIKALI IMEFUTA USAJILI WA VIBALI VYA UZALISHAJI NA UINGIZAJI WA POMBE ZA VIROBA



Serikali imefuta usajili wa vibali vya uzalishaji na Uingizaji wa aina 20 ya pombe kali za viroba zilizokuwa zimesajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo, Jijini Dar es Salaam kuhusu usitishaji wa uzalishaji na uingizaji, uuzaji na matumizi ya pombe zilizofungwa katika mifuko ya plastiki (Viroba).

“Tumefuta usajili wa vibali vya uzalishaji na uingizaji kutoka nje, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zilizofungashwa katika mifuko ya plastiki (viroba) chini ya ujazo wa milimita 200,” alifafanua Ummy Mwalimu.

Aliendelea kwa kusema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa tamko la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilotoa Februari 02, 2017 la kusitisha uzalishaji, uingizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe hiyo kali kuanzia Machi 01, 2017.

Ummy amesema kuwa usitishaji huo unazingatia kanuni za kukataza uzalishaji, uingizaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki kufungashia pombe kali za mwaka 2017 (The Environmental Management (Prohibition of Manufacturing, Important and Use of Plastic Sachets for Packakging Distilled and other alcoholic beverages) Regulations 2017) imekatazwa kutumia vifungashio vya plastiki kufungashia pombe kali. Badala yake wazalishaji watapaswa kufungasha pombe kali hizo katika chupa zenye ujazo usiopungua mililita 200.

Aidha amesema kuwa uamuzi wa kupiga marufuku matumizi ya pombe za aina hiyo unatokana na athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kiafya na kijamii. 

Matumizi mabaya ya pombe hizo yamesababisha  ajali nyingi, vifo, ulemavu na mzigo mkubwa kwa Serikali wa kutoa huduma kwa wahanga wa pombe hizo na ongezeko la makosa ya jinai.


Ummy amesema kwamba Viroba vilivyokamatwa na kuzuiwa vinasubiri maelekezo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu namna ya kuviteketeza.

No comments:

Post a Comment