Tume iliyoundwa kwa
ajili ya kuchunguza kifo cha Faru John imethibitisha kuwa Faru huyo
alikufa katika eneo la Sasakwa Grumeti kutokana na kukosa matunzo, uangalizi wa
karibu na matibabu alipoumwa.
Hayo yamesemwa leo
Jijini, Dar es Salaam na Mkemi Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyele alipokuwa
akikabidhi ripoti ya uchunguzi wa Kifo cha Faru huyo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
“Sampuli
zilizochukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba ni mifupa ambayo
ilichukuliwa katika mzoga wa Faru John uliokutwa eneo la Sasakwa Grumeti, Pembe
zilizochukuliwa hifadhi ya Dar es Salaam na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA), damu kutoka maabara ya NCAA na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine
(SUA), ngozi kutoka kwenye mzoga na kinyesi kilichokaushwa kutoka SUA,”
alifafanua Prof. Manyele.
Aliendelea kwa kusema
kuwa matokeo ya uchunguzi wa awali yameonyesha damu, pembe, mifupa na ngozi ni
vya Faru John ambapo mpangilio wa vinasaba umeonyesho kuwa Faru huyo ni mweusi
(Black Rhinoceros) mwenye jinsia ya kiume.
Aidha vielelezo hivyo
vilitumwa Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini ambapo timu ya wataalam
kutoka Tanzania chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali walishiriki katika
uchunguzi wa awali wa vinasaba na kujadili matokeo kabla ya kuyatuma kwa Mkemia
Mkuu wa Serikali ambapo Matokeo yameonyesha sampuli na vielelezo vyote ni vya
mnyama pori Faru John.
Vile vile amesema,
uchunguzi umeonyesha kuwa sababu za kifo cha Faru huyo ni kukosa matunzo,
uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na
kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria pamoja na mapungufu ya kiuongozi kwa
Wizara, Hifadhi na Taasisi zake.
Baadhi ya mapungufu
yaliyobainishwa katika uchunguzi huo ni pamoja na kutokuwepo na kibali rasmi
kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka NCAA
kwenda Grumeti.
Prof. Manyele amesema
kuwa hakukuwa na mkataba rasmi kati ya Serikali na mwekezaji
unaoonyesha mnyama ametoka Serikalini kwenda kwa Mwekezaji.
Tume hiyo imeishauri
Serikali kuchunguza viwanja vya ndege ndani ya hifadhi
vinavyomilikiwa na wawekezaji kutokana na kuwepo na uwezekano wa viwanja hivyo
kuwa njia ya majangili au matajiri kufanikiisha shughuli za ujangiri
nchini.
Aidha kutokana na
mapungufu ya kiutendaji yaliyofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori
nchini (kutokutoa kibali rasmi) na mapungufu ya kiuongozi yaliyofanywa na
Mhifadhi wa NCAA kuruhusu Faru John kuondolewa bila kibali, Tume inashauri
hatua za kiutawala zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Kwa upande wake,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza timu hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Ameahidi kufanyia kazi maoni ya tume hiyo na kutolea maelezo ya hatua
zitakazochukuliwa na Serikali muda mfupi ujayo.
Tume ya uchunguzi ya
kifo cha Faru John iliundwa baada ya Waziri Mkuu kufanya ziara ya kikazi
Ngorongoro Disemba 6, 2016, ambapo alibaini kuhamishwa kinyemela kwa faru huyo
na kudaiwa kupelekwa Grumeti.
Waziri Mkuu alitaka
ukweli kuhusu upotevu wa Faru huyo na kuamua kuunda tume hiyo ili kubaini
ukweli wa Faru huyo kama alikufa au alitoroshwa.
No comments:
Post a Comment