Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema Kenya ni nchi inayoongoza
kwa uwekezaji nchini Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine za Bara la
Afrika.
Rais Magufuli amesema
hayo leo tarehe 31 Oktoba, 2016 katika mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya ambako ameanza ziara ya
Kiserikali ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru
Kenyatta.
Rais Magufuli ambaye
kabla ya Mkutano huo na waandishi wa habari amepokelewa rasmi kwa kupigiwa
mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na baadaye
kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, amesema takwimu
za kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa Kenya ina jumla ya
kampuni 529 zinazoendesha shughuli zake nchini Tanzania ambapo zimewekeza Dola
za Marekani Bilioni 1.7 na zimeajiri watu 56,260.
Pia, Rais Magufuli
amebainisha kuwa biashara kati ya Tanzania na Kenya imeongezeka kutoka Shilingi
za Kitanzania Bilioni 652.9 hadi Shilingi za Kitanzania Trilioni 2.044.
“Naomba niwahakikishie
kuwa uhusiano na ushirikiano wetu ni mzuri na utaendelea kuwa mzuri zaidi, na
kwetu sisi Tanzania, Kenya ndio nchi ya kwanza kwa uwekezaji kuliko nchi zote
za Afrika.
“Tunashirikiana vizuri
katika uchumi, watu wetu wanafanya kazi pamoja, yapo makabila yetu ambayo
yanaingiliana kwa shughuli zao za kila siku na hata wanyamapori wetu
wanazunguka katika nchi zote mbili bila kujali mipaka” amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli
amesisitiza kuwa Serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na
Kenya ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta na amewakaribisha
wafanyabiashara wengi zaidi wa Kenya kuwekeza nchini Tanzania.
“Kabla ya kuja hapa
nimekwenda kutoa heshima katika kaburi la Mzee Jomo Kenyatta, kwa kweli
nimeguswa sana na kazi kubwa iliyofanywa na wazee wetu, naomba niwahakikishie
kuwa tunawathamini sana ndugu zetu Wakenya na tutaendelea kufanya hivyo” amesisitiza Dkt.
Magufuli.
Kwa upande wake Rais
wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali
mwaliko wake na amemhakikishia kuwa Kenya itaendeleza na kuimarisha zaidi
uhusiano na ushirikiano na Tanzania.
“Kwetu sisi Tanzania
ni ndugu zetu, ni kaka na dada zetu tunao ushirikiano wa siku nyingi na wa
kidugu na tutahakikisha tunauendeleza ushirikiano na uhusiano huu mzuri
ulioasisiwa na wazee wetu” amesema Mhe. Kenyatta.
Rais Kenyatta amesema
Tanzania na Kenya ni nchi zinazofanana kwa mambo mengi muhimu ikiwemo
kubadilishana uongozi wa Serikali kwa njia ya amani na ameongeza kuwa katika
mazungumzo yao wamekubaliana kuwa nchi hizi zitaendelea kuzisaidia nchi
nyingine za Afrika Mashariki zinazokabiliwa na matatizo mbalimbali.
Aidha, Rais Kenyatta
amesema Kenya itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya
ushirikiano ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara ya Bagamoyo
(Tanzania) hadi Malindi (Kenya) pamoja na mambo mengine ambayo Tume ya pamoja
ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili (Joint Commission Cooperation)
itayaainisha.
Baadaye leo, Rais
Magufuli anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa katika Ikulu ya Nairobi
aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta na Kesho anatarajiwa
kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen Jijini
Nairobi, na kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo Jijini
Nairobi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Nairobi
31 Oktoba, 2016
No comments:
Post a Comment