Monday, 10 October 2016

SERIKALI KUHAKIKISHA IDADI KUBWA YA WANANCHI VIJIJINI NA MIJINI KUNUFAIKA NA HUDUMA YA MAJI



Serikali imesema imejipanga kuhakikisha kuwa idadi kubwa ya wananchi waishio vijijini na mijini hapa nchini wananufaika na huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama ili kuwaondolea kero ya uhaba wa maji  watanzania ifikapo mwaka 2020.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge wakati wa uzinduzi wa Bodi ya wadhamini ya Mfuko wa Maji.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuongeza huduma ya upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 72 hadi asilimia 85 na mijini kutoka asilimia 86 hadi asilimia 95 ifikapo mwaka 2020.

Waziri Lwenge amesema ili kufikia lengo hilo Serikali itahakikisha inafanyakazi kwa juhudi na weledi na maarifa ili kuondokana na kero hizo.

Katika kufikia malengo ya Serikali kuwa ifikapo mwaka 2020 huduma ya maji inawafikia wananchi waishio vijijini kwa asilimia 85 kutoka asilimia 72 ya sasa na mijini kwa asilimia 95 kutoka aslimia 86 ya sasa,” alifafanua waziri Lwenge.

Katika kufanikisha hilo Waziri Lwenge ameiagiza Bodi hiyo kuwa wabunifu, waadilifu na wachapakazi ili kuleta mabadiliko ambayo yataiwezesha nchi kuwa nchi ya Uchumi wa kati na ya Viwanda hasa katika Sekta ya Maji.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Mbogo Futakamba alisema kuwa matumaini ya Serikali katika kuimarisha hali ya huduma ya maji vijijini na mjini ni kuona mfuko huo unasimamia ili kutoa matunda yaliyokusudia.

Aidha, Mhandisi Futakamba alisema kuwa Bodi ya Wadhamini imekasimiwa jukumu la kusimamia na kulinda maslahi ya Taifa katika kuhakikisha Sekretarieti ya Mfuko inatekeleza majukumu kwa mujibu wa Sheria, Kanunu na Taratibu zilizopo. 




No comments:

Post a Comment