Sunday, 30 October 2016

TEMESA YAANZISHA PROGRAMU YA KUBAINI VIPURI BANDIA.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (kulia) akisikiliza taarifa ya kituo cha TEMESA Iringa kutoka kwa Meneja wa kituo hicho Mhandisi Ian Makule.
 
Meneja wa TEMESA Iringa Mhandisi Ian Makule (Kulia) akimuonesha Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (kushoto) stoo ya vifaa kwa ajili ya ukarabati mdogo wa magari.
Wakala wa Ufundi na Umeme(TEMESA) imeanzisha program ya kubaini vipuri bandia kwa ajili ya kuboresha huduma za matengenezo ya magari na mashine mbalimbali.

Agizo hilo limetolewa na Mtendaji Mkuu wa TEMESA  Dkt.Mussa  Mgwatu alipotembelea karakana ya TEMESA mkoani Iringa kujionea jinsi karakana hiyo inayotumia kutumia mfumo huo wa kubaini vipuri bandia.

Dkt Mgwatu ameongeza kuwa mfumo huu umekuja wakati sahihi kwani kwa sasa kumekuwa na uingizwaji wa vipuri bandia ambao umesababisha hasara kwa wamiliki wa vifaa vinavyotumia vipuri kutoka nje ya Tanzania.

“Ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia inabidi tuwe na mfumo ambao utatusaidia kutambua vipuri bandia kwani vinakwamisha sana utendaji kazi wetu” alisema Dkt Mgwatu.

Akieleza jinsi mfumo huo unavyofanya kazi, Meneja wa TEMESA Iringa Mhandisi Ian Makule alisema kuwa kwa kuingiza taarifa za namba ya gari husika kwenye program ya kompyuta, unaweza kubaini kama kipuri kinachokusudiwa ni halisi kabla ya kukiagiza.
Mhandisi Makule aliongeza  kuwa kama namba na jina la kipuri zitakuwa sahihi kwenye kasha lake lakini kipuri chenyewe sio halisi, kitaweza kutambuliwa kwa kutumia programu ya ‘barcode scanner’.

Dkt. Mussa Mgwatu ameziagiza karakana zote za TEMESA nchini kuanza kutumia programu ya kompyuta katika kuagizia vipuri toka kwa wazabuni ili kuondokana na lawama zinaotokea wakati wa kutengeneza na kukarabati magari ya Serikali na mitambo mbalimbali.


Soko la vipuri vya magari, kama yalivyo masoko ya vifaa vingine, limeingiliwa kwa kasi na uwepo wa vipuri bandia (Non genuine parts) katika kukabiliana na tatizo hili TEMESA imeamua kuanzisha mfumo wa kubaini vipuri bandia.

No comments:

Post a Comment