Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akiwasilisha kwa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mswada wa Sheria ya Huduma za
Habari 2016 leo Mjini Dodoma Oktoba 18,2016
Serikali imewasilisha
mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii Muswada wa Huduma za
Habari ikieleza kuwa ni sheria itakayoleta mageuzi makubwa nchini.
Hayo yamesemwa na
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa
akiwasilisha muswada wa sheria hiyo leo mjini Dodoma ambapo amesema sasa sekta
ya habari inakwenda kuwa taaluma kamili.
Waziri Nnauye amesema
Sheria hii italeta mifumo ya kisasa ya usimamizi wa sekta ya habari na mifumo
ambayo inaweza kugusa au kubadili namna wanahabari walivyozoea kutenda au
kufikirika kwa sasa lakini akasema sekta hiyo iwe tayari kwa mabadiliko.
“Niwaombe wanatasnia
wenzangu tuwe tayari kwa mabadiliko haya ili taaluma yetu iheshimike na sisi
wenyewe tuheshimike zaidi” alisisitiza Mhe. Nnauye.
Aidha Mhe. Nnauye
ametoa wito kwa wadau wote kuunga mkono muswada huo utakaojadiliwa katika Bunge
lijalo la Novemba mwaka huu.
“Tuko hapa kuboresha
na sio kusuguana tukae tuiandae tasnia bora zaidi kwa kupitia na kutoa maoni
juu ya Muswaada huu wa Sheria ya Huduma za Habari 2016” alifafanua Mhe. Nnauye.
Ameongeza kuwa kwa
sasa hadi wakati wa Bunge lijalo Serikali ipo tayari kupokea na kuyafanyia kazi
maboresho yatakayolenga kufikia maono ya muswada huu kutoka kwa wadau
ili kuipa heshima stahiki sekta ya habari.
Alisema kuwa muswada
huo licha ya huu utatatua changamoto za kutotambulika kwa sekta ya habari kama
taaluma kamili inayopaswa kuheshimiwa, pia utatatua changamoto ya kukosekana
vyombo madhubuti na huru vya usimamizi wa tasnia.
Alisema kutokana na
hayo muswada unapendekeza kuundwa kwa Bodi ya Ithibati itakayoainisha sifa za
mwanahabari na kuwasajili.
Aliitaja taasisi
nyingine inayoundwa kuwa ni Baraza Huru la Wanahabari ambalo litakuwa na wajibu
wa kuandaa na kusimamia maadili ya wanahabari na watawajibishana wenyewe kwa
wenyewe.
Wasomi
wanena
Mhadhiri wa Sayansi ya
Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Benson Bana anasema kuwa kuja
kwa sheria hiyo ni jambo la busara kwa sababu kwa sasa weledi wa uandishi wa habari
uko chini.
“Sheria hii iwe na
makali zaidi kwa wanahabari ambao watakiuka utaratibu na maadili. Hakuna nchi
ambako wanahabari wanajiendea tu bila uratibu,” alisema,
Alisema ni vyema na ni
wakati mauafaka kwa sekta ya habari kuwa taaluma kamili na kushauri kuwa
wanaoitumikia fani hiyo kwa sasa wawe tayari kwa mabadiliko.
Naye Mhadhiri wa
Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt
William John Walwa alisema sheria imekuja wakati muafaka na inapaswa kutatua
changamoto za fani hiyo.
No comments:
Post a Comment