Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan, amekiri kuwapo uhaba wa dawa na vifaa
tiba katika hospitali za Serikali nchini.
Amesema uhaba huo wa
dawa ni changamoto ya muda mfupi na Serikali inatafuta ufumbuzi wa haraka
kuwahudumia wananchi.
Alikuwa
akizungumza Dar es Salaam jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa
wodi ya kina mama na watoto katika hospitali zote za rufaa za Mkoa wa Dar
es Salaam.
Samia alisema
anatambua changamoto zinazoikabili Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, kwamba ni ukosefu wa dawa.
“Natambua katika hospitali zetu za rufaa tuna
changamoto ya vifaa tiba na dawa, lakini Serikali tunaifanyia kazi kila
mwananchi aweze kupata huduma hizo kama ilivyopangwa,”alisema.
Alisema
idadi watu wanaoongezeka katika Mkoa wa Dar es Salaam husababisha msongamano wa
wajawazito na watoto katika hospitali za Serikali na kuwafanya kina mama walale
chini au walale mbali na watoto wao.
“Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni,
takriban wanawake 432 kati ya vizazi hai 100,000, hufa kila mwaka kutokana na
uzazi na asilimia 80 ya vifo hivyo husababishwa na ukosefu wa vifaa tiba,
umbali wa vituo vya afya, upasuaji wa huduma za dharura ya upasuaji kwa
wajawazito na kuongezewa damu.
“Kwa Mkoa wa Dar es Salaam peke yake, kuna
zaidi ya hospitali 42 zinazotoa huduma za dharura za uzazi kwa kasi ya ukuaji
wa jiji na bado Serikali inahitaji zaidi ya hospitali 30 ndani ya miaka 10
ijayo,”alisema.
Kwa mujibu wa Samia,
mradi wa ujenzi huo utagharimu Sh bilioni 4.5 kwa hospitali tatu na kila
hospitali yenye ghorofa tatu na uwezo wa kuwekwa vitanda 150, itagharimu
Sh bilioni 1.2.
Alisema Serikali
imejipanga kuhakikisha hospitali zote za rufaa zinaendelea kuimarishwa ili
kutoa huduma bora za afya ikiwamo afya ya mama na mtoto.
No comments:
Post a Comment