Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (kulia) akisikiliza
taarifa ya Meneja wa TEMESA Geita Mhandisi Gilly Chacha (Kushoto) alipotembelea
kituoni hapo.
Mtendaji Mkuu wa
TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (kulia) akikagua sehemu ya kutengenezea magari
katika karakana ya TEMESA Geita alipotembelea kituoni hapo (aliyevaa
miwani) ni Meneja wa TEMESA Geita Mhandisi Gilly Chacha.
Watumishi wa karakana ya TEMESA Geita wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa
TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (hayupo pichani) alipotembelea kituoni hapo.
Mkuu wa Wakala wa
Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu amewataka watendaji wake katika vituo
vyote vya TEMESA nchini kuanza kujenga mazingira ya kujitegemea na kuondokana
na fikra za kutegemea fedha kutoka Serikalini.
Agizo hilo limetolewa
na Mtendaji huyo alipotembelea karakana ya TEMESA iliyopo mkoani Geita na
kujionea kazi zinazofanywa na karakana hiyo na kuagiza watendaji wake kutafuta
mbinu mbadala ya kuzalisha mapato ili waweze kujiendesha wenyewe.
“Naomba muanze
mikakati ya kufanya kazi kwa kasi na ubora na kuongeza ubunifu ili kuhakikisha
kituo kinakusanya mapato ya kutosha kuweza kujiendesha kwa kuwa serikali hapo
baadae haitaendelea kutoa ruzuku kwa taasisi zake zote zinazozalisha”
alisisitiza Dkt. Mgwatu.
Mtendaji Mkuu huyo
amemuagiza Meneja wa TEMESA Geita kuhakikisha anafanya matengenezo sehemu ya
kutengenezea magari iliyopo kituoni hapo, kuwapa mikataba watumishi wote wasio
na ajira za kudumu, kuhakikisha watumishi wanapata vitendea kazi kulingana na
mahitaji ya kada zao, kufuatilia kwa karibu wadaiwa sugu wa kituo, na
kuhakikisha madeni yaliyopo sasa yanalipwa pamoja na kuongeza uzalishaji wa kituo
hicho.
Kwa upande wake Meneja
wa TEMESA Mkoa wa Geita Mhandisi Gilly Chacha ameeleza changamoto zilizopo kuwa
ni uchakavu wa karakana na vifaa vya kazi pamoja na uwepo wa madeni sugu
wanazozidai Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Halmashauri ya Wilaya ya
Chato na Mbongwe pamoja na ofisi ya Mkurugenzi wa Mji wa Geita.
“Mtendaji tunakuahidi
kuanza kutekeleza agizo lako la kuzalisha mapato zaidi ili tujitegemee na
kutotegemea ruzuku kutoka Serikalini kwa kuwa wabunifu na kujituma katika kazi
na kukusanya madeni yote tunayodai” alisema Mhandisi Gilly Chacha.
Aidha Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu amemtaka Meneja wa TEMESA
Geita kumpatia taarifa za ufuatiliaji wa madeni ya wadaiwa sugu na taarifa ya
mapato yaliyokusanywa na kituo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ili kujua pato
halisi la kituo.
Mtendaji Mkuu wa
TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu yupo katika ziara ya kikazi Kanda ya Ziwa na
atatembelea vituo vya TEMESA vilivyopo ili kubaini changamoto na kujionea
utendaji kazi wa vituo hivyo na sasa yupo Mkoani Geita.
No comments:
Post a Comment