Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza viongozi wote wa
Serikali walioalikwa kuhudhuria sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru
kitaifa zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2016 katika Wilaya ya Bariadi Mkoani
Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao walishalipwa fedha ya posho na
safari kwa ajili hiyo wazirejeshe.
Taarifa iliyotolewa
leo tarehe 12 Oktoba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi
Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Rais Magufuli ametoa maagizo hayo ikiwa ni
utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kubana matumizi yasiyo ya
lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika shughuli za maendeleo ya nchi.
Viongozi waliotajwa
kutakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na Wakuu wote wa Mikoa,
Wakuu wote wa Wilaya, Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mameya
na Wenyeviti wote wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na
watumishi ambao huambatana nao wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa
idadi hufikia takribani 1,500.
Kwa kuwa sherehe za
Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na Maadhimisho ya Siku ya
Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere aliyefariki dunia miaka 17 iliyopita, agizo hilo limewataka Viongozi
wote wa Mikoa na Wilaya kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu
wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.
Aidha, Rais Magufuli
ameagiza Wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika shughuli za maendeleo
wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi
katika siku ya kilele cha Mbio za Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa
zitapelekwa kwa wahusika kwa utaratibu utakaoelekezwa na Mamlaka inayohusika
kutoa zawadi hizo.
Hata hivyo Dkt.
Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa,
Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na Wilaya zake pamoja na wananchi
wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi na kushiriki katika sherehe za kuzima
Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe 14 Oktoba, 2016.
Mgeni Rasmi katika
sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
12 Oktoba, 2016
No comments:
Post a Comment