Mkuu wa wilaya ya Geita Mwl. Herman C. Kapufi
Mauaji ya
walinzi mkoani Geita yamendelea kuwa tishio kwa usalama wao baada ya mlinzi
mwingine aliyekuwa akilinda maduka yapatayo 15, kuuawa kwa kupigwa na kitu
chenye ncha kali kichwani.
Mauaji ya mlinzi huyo
Kisusi Iddy (40) aliyekuwa akilinda maduka hayo kwenye Mtaa wa Mwatulole, ni
muendelezo wa matukio ya kuuawa walinzi wa maduka na mali mbalimbali kwani
katika kipindi cha miaka miwili jumla ya walinzi 20 wameuawa.
Taarifa zilizopatikana
jana kuhusu mauaji ya mlinzi huyo na kuthibitishwa na mwenyekiti wa mtaa huo,
Fikiri Toi zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Januari Mosi na
wauaji hao hawakuiba kitu chochote.
Mwili wa Iddy ulikutwa
umefunikwa kwa shuka lake alilokuwa akilitumia lindoni, huku likiwa limetapakaa
damu.
Kutokana na tukio
hilo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama amefuta vibali vyote vya waganga wa tiba za asili kwa
madai wao ni moja ya chanzo cha imani za kishirikina zinazosababisha mauaji
hayo.
Alisema kutokana
na kukithiri kwa mauaji hayo, mamlaka yake inakusudia kufufua Jeshi la Jadi
(Sungusungu) ili kusaidia kuyadhibiti.
Hata hivyo, Kapufi
alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa wakati wa uhai wake, Iddy alikuwa
analinda maduka ya wafanyabiashara yanayofikia 15 na kwamba baada ya
kufuatilia, hakuwa na mafunzo yoyote ya ulinzi.
No comments:
Post a Comment