Mwanadiplomasia mahiri
wa Tanzania aliyepata pia kuwa Katibu Kiongozi-Ikulu, Balozi Ombeni Sefue
ameteuliwa kuwa Mtanzania wa kwanza kuingia katika Jopo la Watu Mashuhuri
katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji
wa APRM tawi la Tanzania, Rehema Twalib anayehudhuria mikutano ya Umoja wa
Afrika na APRM mjini Addis Ababa, Ethiopia, Balozi Sefue ameidhinishwa kwenye
kikao cha juu ya Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika ambao ni wanachama wa APRM
kilichofanyika juzi Jumamosi mchana.
“Haikuwa kazi rahisi
kupata nafasi hii. Nchi nyingi za Afrika zilileta majina ya watu wao mashuhuri
ili kuingia katika jopo hili muhimu. Balozi Sefue licha ya kuwa na utumishi
uliotukuka kama mwanadiplomasia mkongwe pia aliungwa mkono kwa nguvu zote na
Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania,” alisema Katibu Mtendaji huyo.
APRM ni Mpango wa Afrika
uliobuniwa na Wakuu wa Umoja wa Afrika kwa lengo la kuwa na chombo
kitakachosaidia kuhimiza nchi wanachama kuenzi utawala bora na utoaji wa huduma
bora za kiuchumi, biashara na za kujamii kwa wananchi wao kupitia mfumo wa
kujitathmini zenyewe na kukosoana.
Kwa mujibu wa tovuti ya
APRM, Jopo la Watu Mashuhuri ni chombo cha juu cha kuwashauri Wakuu wa Nchi
Wanachama wa APRM katika uendeshaji wa Mpango huo na husimamia mchakato mzima
wa kujitathmini.
Wajumbe wa jopo hilo
ambao hudumu hadi miaka minne hupendekezwa na nchi zao na baada ya mchakato
mrefu wenye ushindani majina ya waliokidhi vigezo huwasilishwa na kuidhinishwa
na na kikao cha juu katika APRM-Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Tanzania ni miongoni mwa
wanachama 35 kati ya nchi 54 wa Nchi za AU zilizojiunga na APRM na ilijiunga
rasmi na Mpango huo tangu mwaka 2004.Tayari Tanzania ilishafanyiwa tathmini ya
kwanza ya utawala bora na inaendelea kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa.
Katika mkutano huo
Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi za APRM Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aliwapongeza
wajumbe wa jopo hilo na kuwata kushiriki vyema katika kuihuisha APRM na kuwa
chombo chenye thamani kubwa kwa Afrika kama walivyotarajia waasisi wake akina
Thabo Mbeki, Olusegun Obasanjo, Benjamin Mkapa na wengine.
Balozi Sefue ataungana
na wajumbe wengine wapya ambao ni pamoja na Prof. Ibrahim Agboola Gambari
(Nigeria), Balozi Mona Omar Attia (Misri) Bi. Fatma Zohra Karadia (Algeria),
Askofu Don Dinis Salomão Sengulane (Msumbiji) na Prof. Augustin Loada (Burkina
Faso). Wajumbe wa zamani wanaoendelea ni pamoja na Prof. Youssouf Khayal
(Chad) ambaye kwa sasa atakuwa Mwenyekiti wa Jopo hilo na Brigitte Mabandla (Afrika
Kusini) ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti.
Mkutano huo pia
ulijadili Ripoti za tathmini za nchi katika maeneo anuai ya utawala bora kwa
nchi za Kenya (ikiwa ni ripoti ya pili kuwasilishwa), Sudan, Chad, Senegal,
Djibouti pamoja na ripoti ya utekelezaji ya Zambia.
No comments:
Post a Comment