Maduka 14 katika eneo
la Mianzini jijini Arusha yameteketea kwa moto jana asubuhi na kusababisha
hasara mbalimbali huku jeshi la polisi likiimarisha ulinzi na kusimamia
shughuli za uokoaji wa mali zilizosalimika.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Arusha, Charles Mkumbo alisema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme
iliyoanzia kwenye baadhi ya majokofu yaliyokuwa katika baadhi ya maduka
hayo.
Kamanda Mkumbo alisema
mara baada ya hitilafu hiyo, moto huo ulishika mitungi ya gesi iliyolipuka na
kuanza kusambaa kwa kasi na kuunguza maduka hayo.
Alisema wamefanikiwa
kuokoa baadhi ya mali katika maduka tisa kati ya 14 kwa msaada wa wananchi na
wasamaria wema waliokuwa katika eneo la tukio lakini ukubwa wa hasara bado
haujajulikana.
Mmiliki wa moja
ya maduka yaliyoteketea, Zena Athuman alisema kabla ya kufungua biashara yake,
alifika katika eneo la tukio na kukuta moto huo umeshaanza na hakufanikiwa
kuokoa mali yoyote kwa kuwa moto huo ulikuwa ukisambaa kwa kasi ya ajabu.
Shuhuda wa tukio hilo,
Julius Sangeti alisema alifika katika eneo hilo saa 11:30 asubuhi na kushuhudia
moto ukiwaka katika duka kubwa la Mianzini na kadri muda ulivyokuwa ukisonga,
ndivyo ulivyokuwa ukihamia kwenye maduka mengine na kuteketeza mali.
No comments:
Post a Comment