Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT)
Prof.Preksedis Ndomba (kushoto) na Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri
Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Ally Msaki wakisaini makubaliano
ya ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi hiyo utakaowezesha vijana kupata
mafunzo ya uzalishaji wa mazao ya ngozi katika Taasisi hiyo Kampasi ya Mwanza
ili kuchochea uchumi wa viwanda nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam wakati
wa kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano kati ya Taasisi ya Teknolojia Dar
es saalam (DIT) na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu.
Akizungumzia makubaliano hayo Mkurugenzi wa Ajira
kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Ally Msaki
amesema kuwa yatasaidia kuiwezesha Taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa vijana hasa
ya kuzalisha bidhaa zitokanazo na ngozi ili waweze kushiriki katika ujenzi wa
uchumi wa viwanda.
“Vijana 1000 wataanza kupata mafunzo mwezi Februari
mwaka huu na yatakayohusu utengenezaji wa bidhaa za ngozi na program hii ipo
ndani ya mpango wa miaka mitano.” Alisema Msaki.
Mafunzo hayo ya stadi za kazi kwa vijana
yatagharimiwa na Serikali na yatahusisha vijana walio katika mfumo rasmi na
wale wasio katika mfumo rasmi wa elimu lengo likiwa ni kuwakwamua vijana ili
washiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.
Akifafanua Msaki alisema kuwa dhamira ya Serikali ni
kuwawezesha vijana baada ya mafunzo hayo kujiajiri na kuwaajiri wenzao hivyo
kuondokana na tatizo la ajira na kuongeza nguvukazi ya taifa kwenye uzalishaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es
salaam (DIT) Prof.Preksedis Ndomba alibainisha kuwa Taasisi hiyo imejipanga
vyema kuwawezesha vijana kwa kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko na
kuweka msisitizo katika mafunzo kwa vitendo.
Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) ipo
imedhamiria kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga
uchumi wa viwanda na kufikia uchumi wa kati.
No comments:
Post a Comment