Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye
Serikali imejipanga kupitia upya kanuni za utangazaji za Sheria
ya Utangazaji ya mwaka 2003 ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Nape Moses Nnauye wakati wa ziara yake kwa vyombo vya habari vya Channel, na
Tumain Media iliyolenga kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya Serikali na
vyombo vya habari nchini.
Waziri Nape amesema kuwa lengo la mapitio ya kanuni hizo ni
uboreshwaji wa kanuni hizo ili kuisaidia kukuza sekta ya utangazaji.
“Kuna baadhi ya wadau wamekuwa wakilalamika kuhusu kupitwa kwa
wakati kwa kanuni hizo, hivyo tumeona ni vyema kuungana nao ili kuzipitia upya
na kuona palipo na mapungufu” alisema Waziri Nape.
Aidha, Waziri Nape aliongeza kuwa baadhi ya maeneo katika kanuni
hizo yanayohitaji kupitiwa upya ni aina za leseni zilizopo, kubadilika kwa
jamii inayotuzunguka pamoja na mabadiliko ya teknolojia yanayokuwa kwa kasi.
Mbali na hayo Waziri Nape amesema kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa
Mawasiliano Tanzania (TCRA) ipo katika hatua za mwisho za kuandaa kanuni za
kudhibiti masuala ya matumizi ya mitandao ya kijamii nchini.
Katika hatua hiyo Waziri Nape amewataka wadau mbalimbali kutoa
maoni ili kusaidia kuboresha kanuni za mitandao ya kijamii kwa lengo ili kukuza
tasnia ya habari.
Hata hivyo, Waziri Nape ameahidi kuendelea kushirikiana na
vyombo vya habari nchini katika kutoa habari kwa ajili ya kuhabarisha umma
kuhusiana na mambo mbalimbali yahusuyo Serikali katika kutekeleza majukumu
yake.
“Kwa yeyote atakayepata changamoto ya aina yeyote kutoka kwa
watumishi wa Serikali ikiwemo ya upatikanaji wa habari milango ipo wazi katika
kurepoti changamoto hiyo” alisisitiza Waziri Nape.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses
Nnauye yupo katika ziara ya kutembelea vituo vya Televisheni kujionea utendaji
kazi wa vituo hivyo ikiwa pamoja na changamoto zilizopo ili kupata namna bora
ya kuiendeleza sekta ya habari kwa manufaa ya taifa, mpaka sasa ameshatembelea
Kampuni nane za vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment