Mkulima wa tumbaku
aliyesafiri kutoka Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, Moshi Rubibi akitafuta
upenyo wa kumfikishia Rais John Magufuli kilio cha wakulima, alifanikiwa
kufanya hivyo mjini Bukoba wa kutumia staili iliyomvuta Rais
kumsikiliza.
Awali, mkulima huyo
anayewakilisha wenzake zaidi ya 60 alikwama kufanya hivyo wakati Rais Magufuli
alipokuwa kwenye mapumziko wilayani Chato mkoani Geita baada ya kuzuiwa na
walinzi lakini bila kukata tamaa alimfuata Rais mjini Bukoba baada ya kusikia
anafanya ziara.
Utaratibu wa Rais
Magufuli kutaka kusalimiana na wananchi baada ya mkutano ndiyo uliofanikisha
mpango wa mkulima huyo kwani aliamua kupiga kelele mfululizo kwa mbali
akilitaja jina la Rais huku akipunga hewani mkono uliokuwa na bahasha ya kaki.
Pamoja na kudhibitiwa
na walinzi, sauti ya mkulima huyo ilizidi kuchomoza kwa nguvu hali iliyomfanya
Rais Magufuli aliyekuwa anaondoka kwenye eneo la mkutano kupiga hatua kadhaa
nyuma na kuwaambia walinzi wake wamuache amsikilize.
Huku akitweta na
kuhema kwa nguvu baada ya kuruhusiwa kumfikia Rais Magufuli, mkulima huyo
alimwambia kuwa yeye ni mwenyeji wa Urambo, Tabora na amemtafuta ili
kumfikishia malalamiko ya wakulima wa tumbaku wanaopigwa chenga kulipwa mafao
yao.
Alisema wakulima hao
wanadai zaidi ya dola za Marekani 98,000 (zaidi ya Sh200 milioni) za mauzo ya
tumbaku waliyouza kupitia Bodi ya Tumbaku tangu Septemba, 2015 na kuwa
wanashawishiwa kutoa rushwa ili wapewe haki yao.
Alimwambia Rais kuwa
wameambiwa watoe dola 10,983 ili waweze kulipwa fedha zao kupitia tawi la Benki
ya CRDB Urambo na kuwa kati ya kiwango wanachodai cha mauzo ya tumbaku wakubali
kulipwa dola 87,017 tu.
Mkulima huyo alisema
wamefikisha suala hilo kwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo na kukosa ufumbuzi na kuwa
walilipeleka pia kwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo, Mwigulu Nchemba
ambaye alionyesha kuwa tayari kulishughulikia lakini kabla ya kufanya hivyo,
alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Baada ya kumsikiliza
takribani kwa dakika nne, Rais Magufuli alimkabidhi mkulima huyo kwa Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu),
Jenista Mhagama na kuagiza apewe taarifa baada ya siku tano jinsi
walivyoshughulikia suala hilo.
No comments:
Post a Comment