Chama cha Wafanyakazi
wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimevunja ukimya na kuwataka viongozi wa
Serikali, hasa wakuu wa mikoa na wilaya kuacha mara moja kutumia madaraka
yao vibaya dhidi ya wafanyakazi.
TALGWU imesema kuwa
viongozi hao wamekuwa wakitumia kile wanachodai utumbuaji kwa watendaji
kiuonevu na ukiukwaji sheria za nchi.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TALGWU, Rashid Mtima,
alisema baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kama njia
ya kujipatia sifa ama kuonyesha mabavu ya mamlaka yao.
Alisema viongozi hao
wamethubutu kutumia vibaya nafasi zao kwa kuendeleza manyanyaso kwa wafanyakazi
wa kada ya watendaji wa vijiji, mitaa na kata, wakiwaadhibu bila kufuata
utaratibu wa kiutumishi, huku mamlaka zinazopaswa kutumika kwa kazi hiyo
zikiporwa madaraka yake kwa nguvu ya kisiasa.
“Jambo hili ni baya na
la hatari kwa mujibu wa mustakabali wa utawala wa sheria na linapaswa kukemewa
mara moja na kwa nguvu zote kwa sababu likiachwa lina madhara makubwa.
“Tumeshuhudia matukio
ya udhalilishaji na ukiukwaji wa taratibu za kazi wakifanyiwa kada hii, maofisa
watendaji wamekuwa wakiwekwa ndani ovyo kana kwamba wametenda makosa ya jinai,
kutukanwa na kudharauliwa hadharani na wanasiasa, kusimamishwa kazi ovyo bila
kuzingatia mamlaka zao za ajira.
“Kwa mfano Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, aliwaweka ndani watendaji wanne wa Kata ya
Mikocheni kwa kushindwa kutekeleza maagizo yake, vilevile Hapi alipotembelea
Kata ya Kawe aliwaweka ndani watendaji watatu wa mtaa kwa kosa la kuwapa
mashine za kukusanyia fedha wakandarasi na kutounda vikundi vya ulinzi
shirikishi,” alisema Mtima.
Katibu mkuu huyo
alisema kuwa sheria ya tawala za mikoa ya mwaka 1997 inampa mamlaka mkuu wa
mkoa katika kifungu cha 7 (1) hadi (9) na mkuu wa wilaya katika kifungu cha 15
(1) hadi (9) ya kuamrisha mtu yeyote kuwekwa ndani kwa kuona mbele yake au
ufahamu wake mtu huyo kuwa ametenda kosa.
Alisema kifungu kidogo
cha (2) cha sheria hiyo kinamtaka mkuu wa mkoa au wilaya kufanya hivyo pale
ambapo atakuwa amejihakikishia kuwa kosa lililotendwa na mhusika ni lazima
litasababisha uvunjivu wa amani kwa mtendaji na jamii kwa jumla na hakuna njia
mbadala zaidi ya kumuweka ndani.
“Pia kifungu (3)
kinamtaka mtu aliyekamatwa kwa amri au maelekezo ya mkuu wa mkoa au wilaya
afikishwe mahakamani ndani ya saa 48 kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka ya
jinai. Endapo hatofikishwa mahakamani kwa muda unaopaswa na kuisha, anapaswa
kauchiwa na hapaswi kukamatwa tena,” alisema.
Alisema kwa tafsiri
hiyo ya kisheria, ni kwamba viongozi wa kisiasa hawazingatii sheria hiyo
kikamilifu na ni uonevu mkubwa kwa watumishi waliowekwa ndani.
“Swali la kujiuliza
je, uchunguzi ukishakamilika na ikaonekana watendaji waliotangazwa hadharani na
kudhalilishwa walionewa, viongozi hao wa Serikali watatumia vyombo vya habari
kusafisha majina ya watendaji hao?” alisema na kuhoji.
Mtima alisema kuwa
TALGWU haitetei wafanyakazi ambao wanakwenda kinyume na sheria, kanuni na
taratibu za kazi, lakini inataka utaratibu ufuatwe na hatimaye watuhumiwa
wachukuliwe hatua stahiki.
“Wito wetu viongozi wa
kisiasa wenye tabia hiyo watambue dhamana kubwa waliyopewa na Taifa, watumie
mamlaka yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi vinginevyo kama
chama hatutasita kuchukua hatua za kisheria,” alisema Mtima
No comments:
Post a Comment