Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles
Tizeba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula
nchini leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi
Mathew Mtigumwe.
Serikali imesema kuwa hali ya
upatikanaji wa chakula nchini ni ya kuridhisha na kuwataka wananchi kupuuza
taarifa zinazodai kuwa hali ya chakula ni mbaya.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es
Salaam na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji na chakula nchini.
“Ndugu waandishi ukweli ni kwamba hali
ya upatikanaji wa chakula nchini ni ya kuridhisha sana katika maeneo mengi,
hivyo siyo kweli kwamba kuna tatizo la njaa kama baadhi ya watu wanavyojaribu
kupotosha,” alisisitiza Dkt. Tizeba.
Aidha Dkt. Tizeba aliongeza kuwa pamoja
na kuwepo kwa hali nzuri ya chakula, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeendelea kuweka akiba ya chakula kwa kununua jumla
ya tani 62,087.997 za mahindi ili kuhakikisha
nchi inaendelea kuwa na chakula cha kutosha,
Dkt. Tizeba amesema kuwa kwa mwaka wa
fedha 2016/2017 Serikali imejipanga
kununua jumla ya tani 100,000 za chakula ambapo hadi kufikia Januari 8 mwaka 2017 imenunua jumla ya
tani 62,087.997 za mahindi sawa na asilimia 62 ya lengo ililojiwekea.
“Kati ya kiasi kilichonunuliwa, tani
38,162.280 zimenunuliwa kupitia vituo vya ununuzi na tani 23,925.717 kupitia vikundi vya wakulima hivyo hadi kufikia tarehe
12 Januari, 2017 Wakala wana akiba ya tani 88,152.443 za mahindi,” alisema Dkt. Tizeba.
Waziri Tizeba ameongeza kuwa hadi
kufikia katikati ya mwezi Januari, 2017 hali ya chakula na upatikanaji wake
hapa nchini bado ni ya kuridhisha na hasa upatikanaji wa vyakula kama mchele na
maharage ikilinganishwa na zao la mahindi.
Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu,
TAMISEMI, FAO, TFNC pamoja na wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya
kina ya hali ya chakula na lishe nchini ambayo inatarajiwa kukamilika Januari
28 mwaka 2017 na itazihusisha Halmashauri 55, tathmini hiyo itaiwezesha
Serikali kupata taarifa za uhakika zaidi kuhusu hali ya chakula na lishe
nchini.
Amefafanua
kuwa kutokana na hali ya mwenendo wa
unyeshaji wa mvua za vuli na msimu kutokuridhisha katika maeneo mengi ya nchi, Serikali
imewashauri wakulima kutumia mbegu zitakazokomaa mapema na kupanda mazao
yanayostahimili ukame pamoja na kutumia kwa uangalifu na kuhifadhi akiba ya
chakula cha kutosha kwa matumizi katika kaya.
Aidha,
Sekta binafsi zimehamasishwa kuendelea kushiriki katika kutoa masoko ya kununua
na kuuza mazao katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba.
Ufafanuzi
huo umetolewa kufuatia kuwepo kwa taarifa za upotoshwaji juu ya hali ya
upatikanaji wa chakula hapa nchini ambapo Dkt. Tizeba amesema huo ni upotoshaji
wenye lengo la kuwatia hofu wananchi.
No comments:
Post a Comment