Wednesday, 25 January 2017

SERIKALI YASITISHA KUPOKEA WAKIMBIZI WA NCHI ZA MAZIWA MAKUU



Serikali imetangaza kusimamisha kupokea wakimbizi kutoka nchi za Maziwa Makuu kwa makundi, kutokana na kutokuwepo kwa sababu za kiusalama, zinazowafanya wakimbizi hao kukimbia nchi zao na kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametoa kauli hiyo ya serikali mjini Kigoma wakati wa uteketezaji wa silaha haramu, lililofanyika kikanda mkoani Kigoma, na kueleza kuwa kwa sasa hakuna tena wakimbizi watakaoingia kwa makundi watakaoruhusiwa kuingia nchini.

Mwigulu alisema serikali itawapokea wakimbizi mmoja mmoja na kila atakayeingia atahojiwa na mamlaka zinazohusika na mamlaka zikijiridhisha kuwa anastahili hadhi ya ukimbizi, atapokewa na kupelekwa kwenye kambi za wakimbizi zilizopo, kwani hakuna tena kambi ya wakimbizi itakayofunguliwa kwa sasa.

Alisema serikali kwa kutumia vyombo vyake, imejiridhisha kwamba hakuna hali mbaya ya usalama, inayowakimbiza raia hao kutoka kwenye nchi zao na kwamba zaidi imegundulika kuwa wengi wao wanakimbia kwa sababu za kiuchumi, kuja kutafuta namna ya kuishi ili kukidhi hali zao za maisha.

Alisema uwepo na uingiaji wa wakimbizi nchini, umekuwa na mchango mkubwa katika uzagaaji wa silaha haramu sanjari na kuongezeka kwa matukio ya utumiaji wa silaha na kuathiri uchumi na maisha ya watu mbalimbali.

Katika hatua nyingine, waziri huyo amesema serikali imefuta utaratibu wa kutoa uraia kwa makundi, kama ilivyofanya kwa wakimbizi wa Burundi waliopo nchini. Alisema kwamba kwa sasa uraia utatolewa kwa mtu kulingana na maombi yake.

Alisema ukarimu huo wa Watanzania, umekuwa na athari kubwa katika ulinzi na usalama nchini, hasa mikoa ambayo imewahifadhi watu hao kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya mauaji, ujambazi wa kutumia bunduki, lakini kupanda mbegu mbaya ya kuuana kwa kulipiza visasi ambavyo vimekuwa vikifanywa na raia hao waliopewa uraia.

“Kwa mamlaka niliyopewa, natoa amri ya kusimamisha kutoa uraia kwa makundi kama ambavyo imetoa Tanzania na haijawahi kutokea nchi nyingine, tumeona athari kubwa ya watu hao na sasa sehemu kubwa ya Mkoa wa Tabora imekuwa na hali mbaya kiusalama na tabia ya kulipizana visasi,” alieleza Mwigulu.

Akitoa taarifa kwa waziri, Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Marijani Nsato alisema silaha haramu 5,608 zikiwemo bunduki za kivita, zilitarajia kuteketezwa. Nsato alisema katika silaha hizo, kulikuwa na bastola 21, Shortgun 606, SMG 166, Riffle 300, bastola bandia 21, FN Riffle 3, G3 moja, SAR 3 na magobore 4487.

Sanjali na bunduki hizo, aliitaja mikoa ambayo imeshiriki katika kuchangia bunduki haramu zilizoteketezwa kuwa ni Kagera 100, Rukwa 189, Katavi 81, Simiyu 16, Mwanza 88, Geita 82, Mara 80 na Kigoma ukiwa na jumla ya bunduki 424 ambazo zimeteketezwa katika kazi ya jana.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga alisema mkoa huo kuwa mpakani na kupokea idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchi za Maziwa Makuu, kumechangia mkoa huo kuathirika kwa kiasi kikubwa na uzagaaji silaha haramu na matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha.

Alisema mkoa utaendelea kuweka mkakati wa kudhibiti silaha haramu na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha.


No comments:

Post a Comment