Waziri mkuu Kassim
Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Dodoma pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu (CDA) kutenga eneo la bandari kavu ili mkoa huo uweze kupokea na
kuhifadhi mizigo na kurahisisha biashara kwa mikoa jirani.
Ametoa agizo hilo jana
jioni (Jumatano, Julai 20, 2016) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mkoa
wa Dodoma mara baada ya kuweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa awamu ya
kwanza ya ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma.
“Ninazo taarifa kuwa Benki ya Dunia kupitia shirika la Local Investment
Climate (LIC) tayari wametenga fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili
ya kujenga bandari kavu na tayari fedha hizo zimeshapokelewa na Mkoa wa Dodoma
kwa ajili ya kazi hiyo.”
“Uzuri wa mkoa wa Dodoma kuna reli. Kwa hiyo
makontena yanayoenda Burundi na mahali kwingine yatashushwa hapa na kukaa
kwenye bandari kavu; hivyo, wafanyabiashara watachukua mizigo yao hapa badala
ya kupata shida ya kuyafuata Dar es Salaam kama ilivyo sasa,” amesema.
Waziri Mkuu ameitaka
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano itoe wataalam ili washirikiane na CDA
kufanikisha kazi hiyo. Amesema hatua hiyo itasaidia kurahisisha wananchi na
wafanyabiashara kupata huduma hiyo kwa urahisi na umbali mfupi tofauti na hali
ilivyo sasa.
Ameuagiza pia uongozi
wa CDA utenge eneo maalum la kituo cha biashara (commercial hub)) ili Kanda
zote zinazozunguka mkoa wa Dodoma na nchi jirani wapate bidhaa mbalimbali
kutokea Dodoma.
“Kutokana na upanuzi huu na fursa
zinazojitokeza, hii iende sambamba na kuwatengea maeneo maalum wajasiriamali
badala ya kuwaacha kuzagaa kila mahali,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu
upanuzi wa uwanja huo, Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa mradi huo
kutaziwezesha ndege zenye uwezo wa kubeba abiria 90 zianze kutua kwenye kiwanja
hicho na kukuza fursa za kibiashara zinazohitaji usafiri wa haraka na salama.
“Katika Ilani ya CCM, suala la ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya
viwanja vya ndege limepewa umuhimu mkubwa sana na ndiyo maana leo tunashuhudia
utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais ambaye amewezesha upatikanaji wa fedha
za ukarabati na fidia kwa wananchi wa kata za Makole na Uwanja wa Ndege ambao
maeneo yao yametwaliwa na Serikali ili kufanikisha upanuzi huu,” amesema.
Amesema uzinduzi huo
ni mwanzo tu wa utekelezaji wa miradi mingine ya kuboresha na kupanua viwanja
vya ndege nchini ambapo Serikali kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato ya ndani
na ya nje, itaendelea kuboresha zaidi miundombinu na huduma nyingine za viwanja
vya ndege kama vile Mtwara na Mwanza ambavyo amesema vitapanuliwa kufikia hadhi
ya kimataifa.
Ameitaja miradi
mingine kuwa ni viwanja vya ndege vya Kigoma na Tabora ambavyo vinaendelea
kupanuliwa kwa kujenga majengo ya abiria na maegesho ya ndege ili kufikia viwango
vya huduma za kimkoa; viwanja vya Shinyanga na Sumbawanga vitapanuliwa kwa
kuboreshwa miundombinu na majengo yake kufikia hadhi ya viwanja vya kimkoa;
huku kiwanja cha ndege cha Lindi kikiboreshwa miundombinu yake kufikia hadhi ya
kimkoa na kuweza kuhudumia viwanda vinavyotokana na uchumi wa mafuta na gesi.
Amesema Serikali
itaendelea kukamilisha ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal 3) katika
kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ambalo
likishakamilika Desemba 2017 litahudumia abiria wapatao milioni 6 kwa mwaka;
ilhali kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kinapanuliwa
miundombinu yake na jengo la abiria ili kiweze kuhudumia abiria milioni
1.2 kwa mwaka.
Akimkaribisha Waziri
Mkuu kuhutubia hadhara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof.
Makame Mbarawa ameiomba Serikali iendelee kuwekeza katika ujenzi wa uwanja wa
ndege wa Msalato ili ndege za kimataifa ziweze kutua kwenye mkoa huo.
Mapema, akitoa taarifa
ya ujenzi wa mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Dk. Leonard Chamuriho amesema Serikali imetoa sh. bilioni 11.8 kwa
ajili ya kazi hiyo na kwamba hadi sasa wamekamilisha asilimia 60 ya ujenzi kwa
kuweka lami umbali wa km.2.0 kati ya km.2.5 zinazohitaji kukamilishwa chini ya
mradi huo.
Amesema hivi sasa
ndege zinazoweza kuruka na kutua kwa umbali huo zinaweza kuanza kutoa huduma
kwenye uwanja huo wakati wakiendelea kukamilisha ujenzi wa mita 500
zilizobakia.
Kwa upande wake, Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Eng. George Sambali alisema ukarabati huo ulianza Juni
24, 2016 na imechukua siku 27 hadi sasa, kazi ambayo alisema inawezesha
kiwanja kutumika kwa ndege zenye uwezo wa kubeba abiria hadi 90 na zenye mwendo
wa kasi. Hata hivyo, alisema kazi iliyobakia inatarajiwa kukamilika baada ya
miezi miwili.
No comments:
Post a Comment