Tuesday, 26 July 2016

MGOMO DALADALA WASOTESHA ABIRIA MWANZA

Mgomo wa mabasi ya kusafirisha abiria jijini Mwanza leo, umesababisha baadhi ya wakazi wa jiji hilo kutembea umbali mrefu kwa miguu na wengine kutumia usafiri wa vyombo vya usafiri visivyo salama.

Baadhi ya vyombo vilivyotumika ni kama vile malori na pikipiki za miguu mitatu, huku jeshi la polisi likitumia mabomu ya machozi.
Madereva hao waligoma baada ya kulazimishwa na askari wa usalama barabarani kuingia ndani ya kituo cha mabasi nyegezi badala ya kutumia kituo cha Kamanga ambacho kinadaiwa si rasmi.
Mgomo huo ulianza saa tatu asubuhi leo na uliendelea hadi mchana huku wananchi wengi wakilazimika kutembea umbali mrefu kutoka buhongwa kuelekea ilemela, kishiri, igoma na kisesa, wakitumia usafiri wa bajaj na malori.
Rajab Ismail ambaye ni mmoja wa abiria wa usafiri wa daladala jijini hapa, amesema alitembea umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 15, kutokana na kukosekana kwa usafiri baada ya kugoma madereva wake.
Naye mwenyekiti wa chama cha madereva wa daladala kanda ya ziwa, Dede Petro, amelaani kitendo cha askari wa usalama barabarani kuzuia magari kushusha na kupandisha abiria kituo cha Kamanga huku wakitumika askari wa FFU kupiga mabomu kwa lengo la kuwatawanya wananchi.
Amesema kitendo hicho hakifai na kinatakiwa kukemewa na kila mmoja huku akiitaka halmashauri husika kushughulikia tatizo hilo haraka iwezekanavyo na wala wasisubiri mgomo uzidi na kuathiri shughuli za maendeleo kwa wanafunzi na wananchi wengine.
Afisa ukaguzi na ufuatiliaji wa leseni kutoka mamlaka ya udhibiti usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA), Daniel Chilongani, amewataka madereva hao kutumia vituo rasmi vilivyowekwa na mamlaka husika na watafanya vikao kujadili suala hilo.
Chilogani amewaomba madereva wa daladala kurudisha magari barabarani wakati suala lao likishughulikiwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Augustine Senga, aliyekuwapo eneo la tukio, amewataka madereva hao kuendelea na shughuli zao na kuacha kugoma ili kutowasumbua watumiaji wa vyombo hivyo.
Senga alisema badala ya kugoma, wanatakiwa kuendelea na shughuli zao na kutatua migongano na askari wa usalama barabarani kidiplomasia badala ya kugoma.

No comments:

Post a Comment