Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) imesema kupungua kwa mizigo bandarini kumeathiri si Tanzania
pekee bali dunia nzima na kwamba kubanwa kwa mianya ya wizi kumesababisha
kuongezeka kwa mapato kutoka Sh bil 458 Aprili mwaka huu kufikia Sh bil 517.
Akizungumza katika
mkutano na wanahabari jana, Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata alisema upungufu
huo wa mizigo bandarini umezikumba pia bandari za Beira, Msumbiji, Mombasa,
Kenya na kwingineko na kusababisha mapato kupungua.
“Lakini sisi pamoja na
upungufu wa mizigo bandarini makusanyo yanazidi kuongezeka kutokana na kuzibwa
mianya ya kukwepa kodi, hivyo napenda kuwapongeza wafanyakazi wote wa mamlaka
na kusema kwa sasa hakuna mtu anayeweza kukwepa kodi na wale waliozoea wakae
katika njia kuu,” alisema Kidata.
Kidata alisema
wananchi wanatakiwa kuwaunga mkono kwani sasa kodi inaonekana katika kufanya
shughuli za serikali kama kuboresha miundombinu pamoja na kutoa elimu bure.
Alisema TRA imefikia
na kuvuka lengo la makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2015/16 kwa kukusanya
Sh trilioni 13.8 sawa na asilimia 100.04 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 13.4
iliyokuwa imepangwa na serikali.
Kidata alisema katika
kipindi cha Juni mwaka huu, TRA imekusanya Sh trilioni 1.4 sawa na asilimia
107.83 ya lengo la kukuzanya Sh trilioni 1.3 ambapo makusanyo ya mwaka wa fedha
2015/16 ni sawa na ongezeko la asilimia 23.70 la makusanyo ya mwaka 2014/15.
Akizungumzia mashine
za kielektroniki za EFDs, Kidata alisema walipoanza utoaji mashine hizo
zilikuwa 5,703 na mpaka sasa mashine 1,700 zimegawiwa kwa watumiaji na wataanza
kupita duka hadi duka kuhakiki matumizi ya mashine hizo.
Kamishna wa mapato ya
ndani, Elijah Mwandumbya, alisema mwaka huu wa fedha wamejipanga kuhakikisha
wanaondoa changamoto kwa mtu mmoja kuwa na TIN zaidi ya moja hivyo watafanya
uhakiki.
No comments:
Post a Comment