Friday, 22 July 2016

SAMATTA AFUNGA KWA PENALTI GENK YASONGA MBELE EUROPA LEAGUE





 Mbwana Samatta (kushoto) akiruka na kipa wa Buducnost

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ‘Sama Goal’ amefunga penalti ya tatu timu yake, KRC Genk ya Ubelgiji  ikishinda kwa penalti 4-2 dhidi ya wenyeji Buducnost usiku huu Uwanja wa Pod Goricom mjini Podgorica, Montenegro katika mchezo wa marudiano Raundi ya Pili ya mchujo wa kufuzu hatua ya makundi ya Europ League.
Timu hizo zilifikia kwenye matuta baada ya sare ya jumla ya 2-2, Genk ikianza kushinda 2-0, mabao ya Neeskens Kebano kwa penalti dakika ya 16 na Samatta dakika ya 79 Alhamisi iliyopita na usiku huu Buducnost wamelipa kisasi kwa ushindi wa 2-0, mabao ya Radomir Dalovic dakika ya 
kwanza na Milos Raickovic dakika ya 39.

Katika mikwaju ya penalti, mbali na Samatta wengine waliofunga upande wa Genk ni Thomas Buffel, Bryan Heynen na  Dries Wouters ya mwisho, wakati za Buducnost zilifungwa na Risto Radunovic  na Radomir Dalovic, huku Momcilo Raspopovic  na Luka Mirkovic  wakikosa.
Genk ilimaliza mchezo huo pungufu baada ya kungo wake Mghana, Bennard Yao Kumordzi kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 75.

Sasa Genk itamenyana na mshindi wa mechi kati ya BK Hacken ya Sweden na Cork City FC ya Ireland katika Raundi ya Tatu, mechi ya kwanza ikichezwa Julai 28 nyumbani na marudiano Agosti 4 ugenini.
Mchezo wa kwanza baina ya BK Hacken na Cork City FC ulimalizika kwa satre ya 1-1 nchini Sweden. Ikumbukwe timu zitakazoshinda zitakwenda hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi, ambako sasa vigogo kama Manchester United ya England wataanzia huko.
Kikosi cha FK Buducnost Podgorica kilikuwa: Dragojevic, Radunovic, Vukcevic, Vusurovic, Mitrovic, Vujovic/Hocko dk62 Raickovic, Raspopovic, Mirkovic, Janketic/Pejakovic dk52 na Dalovic.
KRC Genk: Bizot, Castagne, Dewaest, Kumordzi, Uronen, Ndidi, Buyens/Heynen dk45, Buffalo, Bailey, Karelis/Wouters dk74 na Samatta.


No comments:

Post a Comment