Friday, 8 July 2016

MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WAONGEZEKA KUTOKA ASILIMIA 5.2 HADI ASILIMIA 5.5


Mfumuko wa bei wa taifa wa mwezi Juni, 2016 umeongezeka hadi asilimia 5.5 kutoka asilimia 5.2 mwezi uliopita kutokana na kuongezeka kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma.
 Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephaim Kwesigabo amesema kuongezeka kwa mfumuko wa bei kumesababishwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi.

“Mfumuko wa bei umesababishwa na kuongezeka kwa bei za vyakula kama vile mahindi ambayo yameongezeka kwa asilimia 3.2, unga wa muhogo kwa asilimia 2.4, samaki wabichi kwa asilimia 3.8, maziwa mgando kwa asilimia 4.3, maharage mabichi yaliyomenywa kwa asilimia 6.1, kitunguu swaumu kwa asilimia 12.5, njegere kwa asilimia 6.2, viazi mviringo kwa asilimia 2.5, mihogo mibichi kwa asilimia 6.7, magimbi kwa asilimia 4.5, na ndizi za kupika kwa asilimia 2.7,” amesema Kwesigabo.

Amesema bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi za bei ni pamoja na huduma ya kinywa na meno ambayo imeongezeka kwa asilimia 13.8, mafuta ya dizeli kwa asilimia 2.4 na mafuta ya petroli kwa asilimia 4.3.

Kwesigabo amesema mfumuko wa bei wa mwezi Juni, 2016 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.5 ongezeko sawa na mwezi uliopita.

Aidha amesema mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwaka wa bidhaa za vyakula majumbani na migahawani umeongezeka hadi asilimia 8.3 mwezi Juni, 2016 kutoka asilimia 7.2 mwezi Mei, 2016. Fahirisi za bei zimeongezeka hadi 103.47 mwezi Juni, 2016 kutoka 103.00 mwezi uliopita.

Kwesigabo amesema uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia Shilingi 96 na senti 65 mwezi Juni, 2016 kutoka mwezi Disemba, 2015.

No comments:

Post a Comment