Wizara imepokea
taarifa kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Shinyanga imevamia ofisi za
shirika la Jhpiego mkoani humo na kukamata baadhi ya watumishi wake kwa madai
ya shirika hilo kugawa mafuta maalumu yanayodhaniwa kutumiwa kuhamasisha ngono
za jinsia moja. Baada ya taarifa hiyo wizara inapenda kutoa ufafanuzi
ufuatao:
Si kweli kwamba
shirika la Jhpiego limekuwa likihamasisha ngono baina ya wapenzi wa jinsia
moja. Shirika hilo kupitia mradi wa “Sauti” linasaidia serikali katika jitihada
za kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa makundi yaliyopo kwenye
hatari kubwa ya maambukizi.
Moja ya makundi
yanayolengwa ni wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao. Shirika limekua
likitoa elimu ya mabadiliko ya tabia kwa wanaume hao huku likiwapatia mafuta
hayo kama sehemu ya kuwasaidia kupunguza hatari ya maambukizi.
Mafuta hayo
yaliingizwa nchini kwa kufuata taratibu za kisheria kwa ufadhili wa Mfuko
Maalumu wa Rais wa Marekani wa kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI
(PEPFAR).
Ndugu wanahabari, kama
mtakumbuka hivi karibuni Wizara kupitia kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu ilisitisha ugawaji wa mafuta hayo
maalumu (vilainishi) miongoni mwa makundi hayo maalumu.
Kufuatia agizo hilo,
Wizara iliagiza Shirika hilo kukusanya mafuta hayo na kuyarudisha katika ofisi
za PEPFAR zilizopo Ubalozi wa Marekani ili yapelekwe katika nchi nyingine
zinazofadhiliwa na PEPFAR ambazo matumizi ya mafuta hayo hayajazuiwa.
Ndugu wanahabari,
Shirika hilo lilitekeleza agizo la wizara la kukusanya mafuta hayo na kuyaweka
katika ofisi zao za kanda, tayari kuyasafirisha kuja jijini Dar es Salaam,
ambapo umeandaliwa utaratibu maalumu wa kuyapeleka katika nchi nyingine bila
kuyaharibu.
Mnamo tarehe 27 mwezi
July, mwaka 2016 Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Shinyanga ilivamia Ofisi za
Shirika hilo na kuchukua mafuta hayo bila kuelewa utaratibu uliotolewa na
Wizara wa kukusanya mafuta hayo na kuyarudisha katika ofisi za PEPFAR.
Zoezi hilo la kamati
ya Ulinzi na Usalama halikushirikisha wizara ya Afya wala wadau wa sekta ya
Afya wilayani humo, ambao wanaelewa vizuri utaratibu uliowekwa na wizara
kukusanya mafuta hayo na kuyarudisha mahali husika bila kuyaharibu.
Ndugu wanahabari,
tayari Wizara imeshamuandikia barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga kutaka
mafuta hayo yaliyochukuliwa kurudishwa katika ofisi za mradi wa Sauti zilizopo
mtaa wa Mwasele, kata ya Kambarage mkoani Shinyanga ili zoezi la kuyakusanya na
kuyarudisha Dar es Salaam liweze kuendelea.
Mwisho, Wizara
inapenda kuwajulisha kuwa shirika la Jhpiego ni miongoni mwa wadau wakuu wa
Serikali ambao wamekuwa wakisaidia huduma mbalimbali za Afya nchini ikiwemo
kusaidia ujenzi wa vituo vya afya, kupambana na maambukizi ya virusi vya
UKIMWI, kuboresha Afya ya mama na mtoto na Uzazi wa Mpango kwa zaidi ya miaka
kumi sasa. Hivyo serikali imeridhia shirika hilo kuendelea kutoa huduma
mbalimbali za afya bila kutumia mafuta hayo.
Imetolewa na:
Michael O. John
Kaimu Katibu Mkuu,
Wiza ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
No comments:
Post a Comment