Tuesday, 5 July 2016

MAJABVI AITEMA SIMBA, AMFUATA MKEWE AUSTRIA


KIUNGO mkongwe wa Zimbabwe, Justice Majabvi hana mpango wa kurejea Simba SC kwa sababu anataka kwenda kumalizia yake soka yake Austria na akaishi huko moja kwa moja.

Habari  zimesema kwamba Majabvi anataka kwenda Austria kuungana na familia yake ambayo inaishi huko.

“Majabvi hataki kurudi Simba, anataka kwenda kwa mkewe Austria akamalizie soka yake na kuchukua uraia aishi moja kwa moja huko. Na jitihada za uongozi kumshawishi arudi zimegonga ukuta kabisa,”kimesema chanzo.

Kwa sababu hiyo Majabvi amewekwa kwenye orodha ya wachezaji wanaoondoka Simba SC na tayari klabu imeanza jitihada za kumsaka mbadala wake.

Justice Majabvi (katikati) hana mpango wa kurejea Simba SC kwa sababu anataka kwenda kuungana na mkewe Austria

Majabvi alijiunga na Simba SC msimu uliopita akitokea Vicem Hai Phong F.C. ya Vietnam ambayo aliichezea kwa msimu mmoja mechi 35 na kufunga mabao matano.

Kisoka aliibukia Lancashire Steel F.C. ya kwao, Zimbabwe mwaka 2002, kabla ya mwaka 2006 kuhamia kwa vigogo wan chi hiyo, Dynamos F.C.

Mwaka 2009 alikwenda LASK Linz ya Austria aliyoichezea mechi 76 na kufunga bao moja moja hadi mwaka 2012 alipohamia Khatoco Khanh Hoa ya Vietnam ambayo aliichezea mechi 28 na kufunga mabao matatu.

Katika kipindi cha msimu mmoja wa kucheza Simba SC, Majabvi mwenye umri wa miaka 32 sasa, amecheza mechi 42 na kufunga bao moja.
Majabvi pia amechezea timu ya taifa ya Zimbabwe mara 27 akifunga bao moja tangu mwaka 2004.


No comments:

Post a Comment