Rais John Magufuli
anatarajia kufanya ziara wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambako atafanya
mkutano wa hadhara kuwashukuru wananchi kwa kumpigia kura nyingi katika
Uchaguzi Mkuu uliopita.
Mkuu wa Wilaya ya
Kahama, Fadhili Nkulu alisema jana kwamba Rais Magufuli atawasili hapa Jumamosi
jioni kabla ya kufanya mkutano wa hadhara Jumapili.
Nkulu aliwataka
wananchi wa Kahama na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kumlaki kiongozi huyo
katika ziara hiyo ambayo alisema: “Lengo lake ni kuwapongeza wananchi
wa Kahama kwa kumpa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika mwaka
jana.”
Alisema ziara hiyo ni
muhimu kwa kuwa ni ya kwanza mkoani Shinyanga akianzia na Kahama.
“Tujipongeze wananchi kutokana na kupata bahati ya wilaya chache zilizotembelewa
na kiongozi huyu, Kahama imekuwa mojawapo,”alisema Nkulu.
Alisema kwa kuwa
Jumamosi ni siku ya usafi kitaifa, kila mmoja wilayani humo ahakikishe anaweka
mazingira katika hali ya usafi na kuwaonya wafanyabiashara kuwa atakayeshindwa
kufanya hivyo hataruhusiwa kufungua biashara.
“Nitafanya ukaguzi Jumamosi kuhakikisha kila mtu anashiriki usafi. Hilo
ni agizo la kitaifa kwa sasa lazima kila mmoja awajibike, nimewaagiza watendaji
wote wa kata kusimamia hilo,” alisema Nkulu.
Alisema wananchi
watatangaziwa ratiba yote ya Rais Magufuli kwenye gari la matangazo ambalo
litazunguka mji mzima wa Kahama kuwaeleza muda na eneo ambalo kiongozi huyo
atafanyia mkutano.
No comments:
Post a Comment