MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ‘Sama Goal’ leo
anatarajiwa kuiongzoa timu yake, KRC Genk ya Ubelgiji katika mchezo wa
marudiano Raundi ya Pili michuano ya Europ League dhidi ya wenyeji Buducnost
nchini Montenegro.
Katika mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Pod Goricom mjini Podgorica, Genk
wanahitaji hata sare au kufungwa kwa tofauti si zaidi ya bao moja ili kusonga
mbele Raundi ya Tatu ya mchujo, baada ya awali kushinda 2-0 nyumbani.
Na ikifanikiwa kuitoa Buducnost, Genk itamenyana na mshindi wa mechi kati ya BK Hacken ya Sweden na Cork City FC ya Ireland katika Raundi ya Tatu, mechi ya kwanza ikichezwa Julai 28 nyumbani na marudiano Agosti 4 ugenini. Mchezo wa kwanza baina ya BK Hacken na Cork City FC ulimalizika kwa satre ya 1-1 nchini Sweden.
Ikumbukwe timu zitakazoshinda zitakwenda hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi, ambako sasa vigogo kama Manchester United ya England wataanzia huko.
Nahodha wa Tanzania, Samatta Alhamisi iliyopita alifunga bao lake la kwanza katika michuano ya Europa League, KRC Genk ikiilaza 2-0 Buducnost ya Montenegro Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
Samatta alifunga bao la pili dakika ya 79, baada ya kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Neeskens Kebano kufunga la kwanza kwa penalti dakika ya 16.
Kocha Mbelgiji wa KRC Genk, Peter Maes alivutiwa mno na Samatta kutokana na kazi nzuri aliyoifanya na akawaambia Waandishi wa Habari; “Ninajivunia Samatta kwa kazi nzuri anayofanya kwa sasa,”.
No comments:
Post a Comment