Saturday, 16 July 2016

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU KUMWAKILISHA RAIS MAGUFULI RWANDA KATIKA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI WANACHAMA WA UMOJA WA AFRIKA (AU).

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassan Suluhu ataondoka nchini leo jumamosi kwenda Kigali nchini Rwanda kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa 27 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Makamu wa Rais atamwakilisha Rais Dkt John Magufuli katika Mkutano huo wa siku mbili ambao unatarajiwa kufanyika Kigali Rwanda kuanzia Julai 17-18 mwaka huu.

Katika Msafara wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassan Suluhu atafuatana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Kikanda na Kimataifa Balozi Augustine Mahiga na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Zanzibar Issa Haji Ussi.

Mkutano huo ambao utahudhuriwa na Makamu wa Rais utaanza kwa vikao vya ndani ambapo viongozi watajikita katika kujadili masuala ya kimkakati ikiwemo umuhimu wa kuliunganisha Bara la Afrika kibiashara kwa kuwa na soko la biashara huria ifikapo mwaka 2017 pamoja na mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Aidha Wajumbe wa mkutano huo wa 27 wa AU pia watachagua Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika pamoja na Makamu wake, Makamishna wanane wa sekta mbalimbali na Majaji wanne wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu pamoja na na kupitisha mapendekezo kuhusu gharama za uendeshaji wa umoja huo na bajeti ya fedha ya mwaka 2017.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassani Suluhu na Ujumbe wake wanatarajia kurejea nchini Julai 19 mwaka huu baada ya kumalizika kwa Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) Kigali nchini Rwanda.

No comments:

Post a Comment