Monday 25 April 2016

WANANCHI MKOANI GEITA WATAKIWA KUCHUKUA VIPIMO KABLA YA KUTUMIA DAWA PINDI WANAPOJIHISI KUUMWA

Ikiwa leo ni kilele cha siku ya maadhimisho ya ugonjwa wa malaria duniani wananchi mkoani Geita wametakiwa  kuacha tabia ya kutumia dawa kabla ya kupata vipimo pindi wanapohisi kuugua na badala yake kufika  katika vituo vya afya ili waweze kupatiwa  tiba sahihi.

Hayo yamebainishwa leo na mratibu wa udhibiti wa malaria mkoani Geita bi Veronica Mazigi alipokuwa akizungumza na Storm habari baada ya kutembelea ofisi za Storm fm zilizopo mkoani hapa.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuachana na dhana potofu ya kudai kuwa vyandarua vinavyotolewa na na mashirika pamoja na wadau mbalimbali vimekuwa vikisababisha upotevu wa nguvu za kiume jambo ambalo halina ukweli wowote.

Aidha bi Mazigi amesema wananchi wanatakiwa  kubadilika kwa kuwa na muitikio chanya kwani ugonjwa huo ni tatizo kubwa kuliko tatizo lingine kitaifa kwa  kufuata utaratibu wanaopewa ikiwa  ni pamoja na kulala katika vyandarua hali ambayo itasaidia kupunguza vifo  vitokanavyo na malaria nchini.

Katika hatua nyingine  maadhimisho ya mwaka huu, wizara ya afya imepanga kuendelea  kutoa elimu kwa jamii juu ya njia mbalimbali  za kijikinga na malaria pamoja na maradhi mengine ya kuambukiza yatakayowajumuisha viongozi wa wizara ya afya, wa mikoa , wilaya na vikundi mbalimbali vya mazoezi pamoja na viongozi wa taasisi za chama na serikali huku  kauli mbiu ya maadhimisho hayo ikisema ‘maliza malaria kabisa’.







No comments:

Post a Comment