Saturday 16 April 2016

RAIS MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA BARABARA YA JUU KATIKA MAKUTANO YA BARABARA ZA NYERERE NA MANDELA JIJINI DAR LEO



Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Eng. Patrick Mfugale akitoa maelezo kwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi ujwenzi wa Barabara ya Juu (FlyOver) kwenye makutano ya Barabara ya Mandela na Nyerere, eneo la Tazara, Jijini Dar es salaam leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza  rasmi ujenzi wa barabara ya juu kwenye makutano ya barabara za Nyerere na Mandela eneo la Tazara jijini Dar es Salaam leo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Magufuli amesema ujenzi huo wa barabara ya juu utaanza mara moja kwa ushirikiano na serikali ya Japan  na utagharimu Shilingi 100 bilioni.

Amesema, serikali ya Japan imefadhili mradi huo kwa Sh 93.44 bilioni wakati serikali ya Tanzania imechangia Sh 8.36 bilioni.

Rais amewataka wananchi watakaopata ajira kwenye ujenzi wa mradi huo wawe waaminifu na wasiwe wezi wa mafuta, vifaa vya ujenzi au kuendekeza migomo.

“Pia serikali ya awamu ya tano imetenga Sh 1 trilioni kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) kwa reli ya kati. Tutajenga kituo kikubwa Ruvu ili mizigo isafirishwe kwa njia ya reli kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Ruvu na malori yatakuwa yakichukua mizigo pale, jambo hili litasaidia kupunguza foleni hapa Dar es Salaam,” alisema Rais Magufuli.

Aidha ameishukuru serikali ya Japan kwa ufadhili wa miradi ya maendeleo nchini kwa zaidi ya miaka 36. Amesema Japan imekuwa ikiisaidia Tanzania bila masharti kama ilivyo kwa baadhi ya wafadhili wa maendeleo. 

Akionyesha kukerwa na wafadhili wanaotoa misaada yenye masharti na vitisho, Rais Magufuli amesema; “Ni bora kula muhogo wa kujitafutia kuliko kula mkate kwa masimango.”

Mbali na mradi huo, Rais amesema serikali yake pia itajenga barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze ambayo itakuwa na barabara za juu tano.

Pia amewataka Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, Wakuu wa Wilaya na Mameya kuhakikisha jiji la Dar es Salaam linakuwa safi muda wote na wachafuzi wa mazingira wachukuliwe hatua za kisheria. 



No comments:

Post a Comment