Sunday 10 April 2016

MSAFARA WA RAISI MAGUFULI KUTOZIDI WATU 10 BALOZI MAHEGA ASEMA ANATEGEMEA KWENDA NG'AMBO HIVI KARIBUNI



Rais John Magufuli anatarajia kusafiri tena kwenda nje ya nchi hivi karibuni akiwa na msafara ambao unawezekana usizidi jumla ya watu 10.

Ilimchukua Rais Magufuli siku 153 tangu kuapishwa kwake kufanya ziara ya kwanza ya nje ya nchi baada ya kwenda Rwanda kwa mwaliko wa Rais Paul Kagame Jumanne iliyopita.

Rais alikwenda Rwanda kwa ajili ya kufungua daraja la kimataifa la Rusumo na kituo cha biashara chenye huduma za pamoja, ambacho ni kiunganishi muhimu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika safari hiyo, katika kile kinachoonekana kuwa ni muendelezo wa hatua yake ya kubana matumizi ya serikali kadri iwezekanavyo, Rais Magufuli alikuwa na msafara usiozidi watu 10.

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustino Mahiga, alisema jana kuwa Rais Magufuli anatarajia kusaifiri tena kwenda nje ya nchi hivi karibuni.

Balozi Mahiga alisema katika safari hiyo, msafara wake utaendelea kuhusisha watu wachache wenye umuhimu katika safari husika ili kuepukana na gharama zisizokuwa za lazima.

Hata hivyo, Balozi hakutaja nchi hiyo itakayofuatia baada ya ziara ya Rwanda wala siku ya kusafiri.

Rais atasafiri tena hivi karibuni… na utaratibu huu wa kuwa na msafara wa watu wachache hautabadilika,” alisema Balozi Maiga.

Akiwa Rwanda, Rais Magufuli alisema hapendi kusafiri kwenda ughaibuni kwa sababu anapenda kubana matumizi kwa vitendo.

Akizungumzia kauli hiyo, Mahiga alisema ni kweli, mara zote Rais Magufuli amekuwa akisisitiza juu ya umuhimu wa kila mmoja ndani ya serikali yake kubana matumizi yasiyokuwa ya lazima na ndiyo maana amekuwa akilidhihirisha hilo kwa vitendo.

Rais anachosema kuhusu kubana matumizi ni kweli kabisa… ndiyo maana msafara wake katika ziara hiyo (ya Rwanda) hatukuzidi watu kumi. "Hii inamaanisha hataki kuwapo kwa matumizi makubwa katika safari za nje.”

Aidha, Balozi Mahiga alifafanua kuwa baadhi ya mawaziri na maafisa wengine kadhaa walioshiriki shughuli ya uzinduzi wa daraja la Rusumo waliishia hapo na kurudi wakati yeye na maafisa wachache wa serikali wakiongozana na Rais katika ziara ya Rwanda.

“Nafikiri mliwaona baadhi ya mawaziri pale Rusumo… wale walitokea huku Tanzania na kurudi. Hawakuwamo katika msafara uliokuwa Rwanda
,” alisema Balozi Mahiga.

No comments:

Post a Comment