Wednesday 27 April 2016

MWANZA YAOKOA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI MOJA KWA KUBANA MATUMIZI

Halmashauri ya Jiji la Mwanza, imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 1 baada ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima tangu mwezi Januari mwaka huu na kuzielekeza fedha hizo kwenye utengenezaji madawati 6,840.
 Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Adam Ngowi, amesema uamuzi wa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ulifikiwa ili kutekeleza agizo la rais Dkt. John Magufuli linalotaka ifikapo Juni 30 mwaka huu tatizo la madawati liwe limemalizika.

Ngowi amesema wanafanya utengenezaji wa madawati hayo ili kupunguza pengo la madawati 11,400 ambalo linasababisha wanafunzi zaidi ya elfu thelathini kujifunza wakiwa wamekaa chini katika halmashauri hiyo.

Aidha, amesema kuwa katika utatuzi wa changamoto hiyo wanakumbwa na changamoto ya upatikanaji wa vifaa ikiwemo mbao hali ambayo inafanya utengenezaji wa madawati hayo kwenda taratibu.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Nyamagana, Baraka Konisaga ametembelea kuona hali halisi ya utengenezaji wa madawati hayo na kusema kuwa kutokana na changamto hiyo wanaweza kufanikiwa kutatua tatizo hilo lakini sio kwa muda ambao wamepangiwa.

Konisaga amewataka wakazi wa wilaya ya Nyamagana kila mmoja wao kwa nafasi yake achangie jitihada hizo za kukamilisha madawati ili kuendana na muda uliopangwa na rais kukamilisha zoezi hilo.

No comments:

Post a Comment