Tuesday 12 April 2016

KAMANDA WA POLISI MWANZA, VIGOGO WA USALAMA WAPANGULIWA

Kamanda wa Polisi, Justus Kamugisha. 
Serikali imepangua uongozi wa vyombo vya dola mkoani Mwanza kwa kuwahamisha vituo vya kazi watendaji wakuu akiwamo Kamanda wa Polisi, Justus Kamugisha aliyehamishiwa mkoani Mbeya.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha utendaji wa taasisi hizo na kukabiliana na matukio ya uhalifu yaliyotikisa mkoa huo tangu kuanza kwa mwaka huu.
“Kwa kipindi kifupi cha wiki mbili tangu nihamie Mwanza, nimeshuhudia matukio kadhaa ya uhalifu, yakiwamo mawili ya ujambazi yaliyoishia kwa raia wema kupoteza maisha na mamilioni ya fedha kuporwa,” alisema Mongella. “RPC amehamishiwa Mbeya ambako nadhani labda kuna changamoto kidogo kulinganisha na zile za Mwanza alizoonyesha kushindwa,” alisema Mongella.
Mongella alisema pamoja na RPC, vigogo wengine waliohamishwa kutoka Mwanza ni pamoja na ofisa utumishi wa jeshi la polisi, ofisa Idara ya Usalama wa Taifa na kamanda wa mkoa wa Idara ya Uhamiaji.
Akizungumza na viongozi, watumishi na watendaji wa vyombo vya dola wilayani Magu, Mongella aliwataka kutimiza wajibu kwa kudhibiti na kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika maeneo yao, akionya watakaoshindwa watawajibishwa.
“Haiwezekani majambazi yatambe kwa kuvamia, kupora na kuua wananchi watakavyo, na vyombo vya dola na viongozi wenye dhamana ya ulinzi na usalama wapo wanashuhudia. Kila mtu atimize wajibu wake,” alisema Mongella.
Alitumia fursa hiyo kuuagiza uongozi wa polisi wilaya ya Magu kukomesha matukio ya mauaji ya kukata watu kwa mapanga yanayodaiwa kufanywa na watu wanaodishwa.
Ndani ya kipindi cha miezi miwili ya Februari na Machi, Jiji la Mwanza limekumbwa na matukio sita ya ujambazi ambayo yamechukua maisha ya watu sita waliouawa kwa kupigwa risasi, huku mamilioni ya fedha yakiporwa kutoka maduka ya fedha kwa njia ya mitandao.
Msemaji wa polisi, Advera Bulimba ambaye awali hakupatikana kuzungumzia suala hilo alituma ujumbe wa simu akieleza kuwa RPC wa Mwanza ni Ahmed Msangi, kwa upande wake Kamanda Kamugisha hakupatikana ila Msangi, ambaye alikuwa kamanda wa Mbeya naye alithibitisha uhamisho huo.
“Ni kweli nimehamishiwa Mwanza na nitafika wakati wowote,” alisema Kamanda Msangi alipozungumza kwa njia ya simu na Mwananchi jana.
Akizungumzia matukio hayo, Mchungaji wa Kanisa la Gosheni Inland Church, Hosea Mjulizi, ambaye ni mkazi wa Igogo, alisema baadhi yanayotokea ni kutokana na vyombo vya dola na viongozi kupuuza taarifa zinazotolewa na wananchi.
“Mfano hai ni Kata ya Igogo ambayo ni kati ya maeneo yanayoongoza kwa uhalifu jijini Mwanza. Licha ya wahalifu kujulikana kwa majina, nyumba zao na matukio waliyohusika, hawachukuliwi hatua,” alisema Mchungaji Mjulizi.
Alisema kwa nafasi yake ya uongozi wa kiroho, alifanya mikutano kadhaa na vijana wanaotuhumiwa kujihusisha ambao walikuwa tayari kujisalimisha, lakini viongozi wa eneo hilo na Jeshi la Polisi hawakutoa ushirikiano.

No comments:

Post a Comment