Friday, 19 January 2018

ZAIDI YA MILIONI 200 KULIPWA NA MGODI WA NYARUGUSU KUFIDIA WANANCHI

DSC_0379
Wananchi wa Kijiji cha Kisiwani Kata ya Nyarugusu ambao mazao yao yaliharibiwa na sumu iliyotoka kwenye Bwawa la kuhifadhia kemikali wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya wakati alipokuwa akitoa maelekezo ya namna ambavyo watalipwa fidia zao.

DSC_0387
Mkuu wa wilaya ya Geita,Mwl Herman Kapufi akielezea mikakati ya namna ambavyo wananchi hao watakavyo lipwa fidia zao na mgodi wa Nyarugusu.

DSC_0395
Mthaminishaji wa serikali,Bw Bahati Albert akionesha taarifa ya uchunguzi na tathimini ilivyofanyika mbele ya wananchi.

DSC_0594
Bwawa la maji ambalo lilimomonyoka na kutililisha maji kwenye mashamba ya wananchi.

Na,Joel Maduka,Geita.


 Wakazi 50 wa Kitongoji cha Mawemeru Kijiji cha Ziwani Kata ya Nyarugusu Wilayani Geita wanatarajiwa kulipwa fidia ya Sh Milioni 200 kutokana na uharibifu wa mazao yao uliosababishwa na sumu iliyotiririka kutoka kwenye Bwawa la kuhifadhia maji yenye Kemikali kwenye mgodi wa Nyarugusu Mine Co.Limited.

Hatua hiyo imekuja baada ya hivi karibu Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Bw Kangi Lugola kuutaka mgodi huo kufanya tathmini kujua kiasi cha hasara iliyosababishwa na sumu hiyo kasha wananchi walipwe fidia.

Bw Bahati Albert ambaye ni mthamini wa mazao yaliyoharibika amesema fidia ya kila mmoja italipwa kutokana na ukubwa wa eneo lake na thamani ya mazao yaliyoharibika kutokana na sumu na kwamba mwekezaji anatakiwa kulipa jumla ya kiasi cha Sh milioni  mia mbili na mbili na laki saba na elifu ishirini na tisa.

Mkuu wa wilaya ya Geita Mwl Herman Kapufi amewataka wananchi wanaotarajiwa kulipwa fidia kutambua kuwa fedha hizo zitalipwa kwa utaratibu wa Benki na sio kupewa mkononi kama wanavyodhani baadhi ya watu.

Mtendaji wa Kata hiyo Bw Thobias amewashauri wananchi hao kutoyavuna mazao hayo kwa kuwa yana sumu na kwamba atakayekamatwa atashughulikiwa kisheria.

Mkurugenzi wa Nyarugusu Mine Co.Limited Bw Fred Masanja amesema kampuni yake inaamini kuwa mthamini amefanya kazi yake kulingana na kila mmoja kwenye eneo lake na kwamba tafiti nyingine zitakuja baadaye.

No comments:

Post a Comment