Serikali Mkoani Geita imewataka wananchi ambao wameendelea kujitolea
kwenye shughuli za maendeleo hususani ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na
shule kuendelea na juhudi hizo na kwamba Serikali ipo pamoja nao kuunga
jitihada hizo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Geita mhandisi Robert Luhumbi wakati
akizungumza na wakazi wa kijiji cha Bukuru Kata ya Kafita Wilayani Nyang’hwale
kwenye kampeni aliyoianzisha ya kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati na
kituo cha afya ifikapo Desemba mwaka huu.
Alisema serikali inatambua juhudi zinazoendelea kufanywa na baadhi ya
wananchi wenye mapenzi mema na kwamba serikali hipo nao bega kwa bega
kuhakikisha inawasaidia kutimiza malengo ambayo wamejiwekea kwenye maeneo yao.
Akisoma taarifa ya uanzishwaji wa zahanati ya Kijiji hicho kwa niaba ya
mtendaji Mwl Timotheo Daniel Njogomi alisema hatua hiyo imekuja baada ya
kukosekana kwa huduma za afya na kuwalazimu wananchi kutembea umbali mrefu
kutafuta huduma hizo hali ambayo imeendelea kupelekea waakina mama wajawazito
kujifungulia njiani.
Bw John Isack ambaye ni diwani wa kata hiyo alisema amekuwa akishirikiana
na viongozi na wananchi wengine katika kujenga zahanati kwenye vijiji vya kata
yake ambavyo bado vinachangamoto kubwa zaidi.
Sanjari na hayo Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Bw Hamim Gweyama amewataka
watumishi kutumia vema fedha za miradi zinazopelekwa kwenye maeneo yao.
No comments:
Post a Comment