Wednesday, 24 January 2018

NHIF WAKABIDHI MAGODORO,VITANDA NA MASHUKA HOSPITALI YA RUFAA YA GEITA

1
 Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bi. Anjela Mziray akionesha vifaa vya msaada vilivyotolewa na Mfuko huo katika Hospitali Teule ya Mkoa wa Geita kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi  Robert Luhumbi.Mapema leo 
2
 Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi  Robert Luhumbi akipokea vitanda 20, magodoro 20 na mashuka 80 msada ambao umetolewa na NHIF.
3
 Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi  Robert Luhumbi  akikalia kitanda kwa lengo la kukagua ubora wake.
4
 Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi  Robert Luhumbi akichunguza kitanda hicho na kuangalia ubora wa mashuka yaliyokabidhiwa.
5
 Baadhi ya Watumishi wa Hospitali hiyo wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa katika hafla ya kukabidhiwa kwa vifaa hivyo.
6
 Meneja wa Mkoa wa Geita wa NHIF, Dk. Mathias Sweya akielezea shughuli zinazofanywa na Mfuko mkoani humo.
7
 Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bi. Anjela Mziray akizungumza na Mama ambaye ni mmoja wa wanachama wa Mfuko.
8
Mkuu wa Mkoa wa Geita Injinia Robert Gabriel wakiwa na Maofisa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Na,Joel Maduka,Geita.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Injinia Robert Gabriel ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa namna ulivyojipanga na unavyoshirikiana na Uongozi wa Mikoa mbalimbali kwa lengo la kuimarisha na kuboresha huduma za matibabu nchini.

Pongezi hizo amezitoa leo wakati akipokea msaada wa vifaa mbalimbali vilivyotolewa na Mfuko katika Hospitali Teule ya Mkoa wa Geita. 

“NHIF nawapongeza sana kwa namna ambavyo mmekuwa tayari wakati wote kuhakikisha huduma za matibabu zinakuwa bora zaidi na niwahakikishie tu kwamba Mkoa umejipanga kutoa huduma kwa wananchi ambazo ni za kiwango cha juu kwani kama viongozi tuna deni la kuwatumikia Watanzania,” alisema

Injinia Gabriel aliutaka Mfuko kutochoka kutoa misaada kama hiyo ambayo inalenga kuwanufaisha wananchi moja kwa moja.

Alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. Pombe John Magufuli imedhamiria kusogeza huduma kwa wananchi hivyo Mkoa unatekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za matibabu ili kuondokana na changamoto za huduma za afya.

Akikabidhi msaada huo, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti, Bi. Anjela Mziray alisema jukumu kubwa la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa Watanzania kupitia mfumo wa bima ya afya.

“NHIF inayo mipango mbalimbali ya kuhakikisha huduma za matibabu zinawafikia wanachama na wananchi kwa ujumla katika mazingira ambayo ni bora zaidi, mipango hiyo ni pamoja na mpango wa Mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ya vituo vya kutolea huduma ambayo ni mikopo nafuu inayosaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha huduma za matibabu,” alisema.

Alisema kuwa NHIF pia imekuwa na mipango mingine ikiwemo ya kupeleka Madaktari Bingwa katika mikoa mbalimbali kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa huduma za kitalaam katika maeneo yote ambapo Mkoa wa Geita ni moja ya Mikoa ambayo imeshanufaika na mpango huo.

Alitumia fursa hiyo kuuomba uongozi wa Mkoa hususani wa Hospitali kuhakikisha unaunga juhudi za Mfuko kwa kuhakikisha unatoa huduma bora kwa wanachama wake na kutatua kero ambazo wamekuwa wakizipata wakati wa kupata huduma hizo.

Bi. Mziray kwa niaba ya Uongozi wa Mfuko alikabidhi Vitanda 20, Magodoro 20 pamoja na mashuka 80 kwa hospitali hiyo ambayo ilikuwa na uhitaji wa vifaa hivyo.

Wakizungumza kwa nyati tofauti wanachama wa Mfuko waliokuwa hospitalini hapo walisema kuwa, huduma wanazopata kupitia kadi za matibabu za NHIF ni nzuri ambazo zimewaondolea usumbufu wa kutafuta fedha wakati wanapopatwa na magojwa.

No comments:

Post a Comment